Kindiki: Michango yetu si hadaa za kisiasa, maisha ya Wakenya yameanza kuimarika
NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki ametetea michango ambayo inaendelezwa na viongozi wa Kenya Kwanza, akisema si hadaa ya kisiasa bali wanalenga kuimarisha maisha ya Wakenya.
Profesa Kindiki alisema matunda ya mikutano hiyo ya kuchangisha pesa imeanza kuonekana kwa sababu makundi ya wanawake na vijana wameanza uwekezaji na maisha yao sasa yameimarika.
“Hizi ni pesa za kibiashara si za kununua nguo au mkate sokoni. Lengo la kuchangishia makundi ya akina mama na vijana ni kuimarisha mapato na maisha yao,” akasema Profesa Kindiki.
“Lengo letu ni kuwainua wanawake na hivi karibuni hata vijana wataona matunda yake,” akaongeza naibu rais.
Alikuwa akiongea katika Shule ya Msingi ya Moi Kabartonjo, Kaunti ya Baringo ambapo alichangishia kundi la akina mama Sh1.2 milioni.
Kando na mchango wake, Profesa Kindiki alitangaza kuwa Rais William Ruto alikuwa ametoa mchango wake wa Sh3 milioni kwa makundi hayo ya akinamama.
Kauli ya Profesa Kindiki ilikuja wakati ambapo viongozi wa upinzani wameshutumu wenzao wa serikali kwa kutumia michango hiyo kusukuma ajenda za kisiasa badala ya kuwapa maendeleo halisi.
Wakati wa hafla hiyo Profesa Kindiki aliahidi kuwa serikali itafufua miradi ya maendeleo iliyokwama na kuzindua mingine mipya.
Alisema miradi mingine ilikwama kutokana na uchechefu wa kifedha ambao ulisababishwa na nyakati ngumu kiuchumi.
“Miradi mingi ikiwemo barabara zilikwama kutokana na ukosefu wa hela. Sasa tuna rasilimali ya kutosha na kazi itaendelea huku miradi mipya ikianza kutekelezwa Baringo,” akasema Profesa Kindiki.
Kati ya barabara ambazo alisema sasa zitatengenezwa ni Kipsaraman-Kinyach, Kinyach-Kolowa-Kamusino kisha Chemolingot-Kapedo-Lokori-
Kuhusu uchaguzi mdogo wa useneta Baringo, Profesa Kindiki aliahidi kuwa mchujo utakuwa huru na haki na mwaniaji anayeungwa na wananchi ndiye atapeperusha bendera ya UDA.
“Kwa unyenyekevu nawaomba muunge mkono atakayekuwa mwaniaji wetu kwa sababu nyinyi ndiyo mtaamua wakati wa uteuzi,” akasema Profesa Kindiki.
Alikuwa ameandamana na Kiongozi wa Wengi kwenye Seneti Aaron Cheruiyot ambaye alisema kuwa serikali haitetereshwi na kukashifiwa na upinzani na badala yake itamakinikia miradi ya maendeleo kwa raia.