• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 8:55 AM
Kindiki- Zaidi ya baa na vilabu 18, 000 vimefungwa

Kindiki- Zaidi ya baa na vilabu 18, 000 vimefungwa

NA WYCLIFFE NYABERI

SERIKALI imefunga vilabu 18, 650 vya kuuza vileo katika vita vinavyoendelea dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya.

Kati ya idadi hiyo, baa 6, 500 zilikuwa na leseni halali lakini ilibainika baa hizo zilikuwa zikikiuka sheria zinazodhibiti pombe.

Vilabu vingine 12, 150 vilivyofungwa vilikuwa havina leseni.

Viwanda vingine 14 vinavyotengeneza pombe ya “makali” kwa kutofuata sheria za nchi pia vimefungwa kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Profesa Kithure Kindiki.

Akizungumza katika ziara yake katika Gereza Kuu la Kisii Jumatatu asubuhi, Machi 25, 2024 Waziri alisema wakati huu serikali imedhamiria kutokomeza tishio hilo kabisa kutumia sheria kwa udhabiti.

“Zamani kila tulipokuwa tukifanya hivi, tulikuwa tukifanya kwa miezi michache tu kisha tunarejelea hali ya kawaida. Lakini safari hii, tumeamua kuendeleza vita kwa misingi ya kudumu jinsi tulivyoendeleza vita kuhusu matishio mengine makubwa ya usalama wa taifa,” Prof Kindiki alisema.

Waziri huyo aliongeza, “Vinywaji vyenye sumu na dawa nyinginezo vinaangamiza watu wengi zaidi wa Kenya. Wanafanya vijana wetu kutokuwa na tija kijamii na kiuchumi. Wanafanya viwango vya uhalifu kuwa vya juu na ninataka kuthibitisha kwamba tangu tuanze msako Machi 7, tumeandikisha kupungua kwa uhalifu unaoripotiwa kote nchini.”

Prof Kindiki aliwataka Wakenya, na hasa vijana kujihusisha na shughuli nyingine za uzalishaji mali badala ya kupoteza maisha yao kwa matumizi ya dawa za kulevya.

Prof Kindiki alisema kisingizio cha ukosefu wa ajira hakiwezi kutumika kuidhinisha aina ya tabia iliyokuwa ikishuhudiwa miongoni mwa vijana mijini na vijijini.

Katika gatuzi la Kisii, Waziri alibaini kuwa washukiwa 95 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kufuatia msako unaoendelea nchini kote.

“Pia tumetwaa karibu lita 40,000 za vinywaji haramu vya sumu. Pia tumeweza kuteketeza viwanda na majengo kadhaa haramu yaliyokuwa yakiuza vinywaji haramu,” Prof Kindiki aliongeza.

Waziri huyo alitumia fursa hiyo kujibu visa vya uhuni ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika mikutano ya kisiasa katika eneo la Kisii na kuonya wanaoendesha fujo hizo kuwa sheria itawakabili hivi karibuni.

“Hakuna mtu atakayeruhusiwa kuvunja sheria kwa kuvuruga mikutano ya hadhara. Hao viongozi wanaotumia vijana wetu kuleta fujo na vurugu kwenye mikutano tunasema wote tutawakamata,” Prof Kindiki alisema.

Alifichua kuwa uchunguzi unaendelea na kwamba hivi karibuni kamatakamata ya wale ambao wamekuwa wakishabikia na kufadhili ghasia za kisiasa itazinduliwa, ili iwe funzo kwa wengine.

“Hakuna aliye juu ya sheria. Kama wasimamizi wa usalama, hatuvutiwi na ushawishi wa kisiasa wa mkosaji. Ukivunja sheria, haijalishi ushawishi wako kisiasa, tutakukamata,” Waziri Kindiki aliongeza.

Waziri huyo alisema mipango ya kuhamisha Gereza Kuu la Kisii nje ya mji inakaribia kukamilika na akaomba serikali ya kaunti ishirikiane nao ili shughuli hiyo iende vyema.

Uamuzi wa kuhamisha kituo hicho cha kurekebisha tabia ulifikiwa baada ya Rais William Ruto kuingia mamlakani, ili ardhi zaidi ipatikane kwa upanuzi wa mji wa Kisii.

Iwapo yote yatafanyika kulingana na mipango iliyowekwa, gereza hilo litaanzishwa katika eneo la Nyanturago eneobunge la Nyaribari Chache.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa 12 mbaroni kwa kupatikana na chang’aa

Himizo watu watumie nguvu za umeme kufanya mapishi

T L