Kingi aita maspika wa kaunti kuwafunza kuhusu sheria ya kuwatimua magavana
SPIKA wa Seneti na Mabunge ya Kaunti wanatarajiwa kukutana baadaye mwezi huu kujadiliana kuhusu kufeli kwa michakato ya kutimuliwa kwa magavana ambayo huchangiwa na sheria kutofuatwa kikamilifu.
Mkutano huo unakuja wakati ambapo kumekuwa na uhasama wa kisiasa kati ya magavana na madiwani ambapo baadhi ya magavana waliotimuliwa bila sheria kufuatwa, wamenusurika.
Gavana wa Isiolo Abdi Guyo mnamo Julai mwaka huu alinusurika kutimuliwa afisini wakati ambapo madiwani walishindwa kutoa ushahidi kuwa waliandaa kikao naye na kumpa muda wa kujitetea.
Baadaye, Gavana wa Kericho Eric Mutai kwa mara ya pili alinusurika kuangushiwa shoka baada ya madiwani tena kushindwa kufuata sheria katika kuondolewa kwake.
Ni kutokana na hili ambapo Spika wa Seneti Amason Kingi ameitisha mkutano pamoja na maspika wa mabunge ya kaunti ili kulainisha mchakato wa kuwabandua magavana ili ufuate sheria na kuondoa mategu ya kisheria ambayo hutokea.
Bw Kingi alisema kuwa kutimuliwa kwa magavana kunaongozwa kisheria ambazo madiwani lazima wafuate kabla ya kufanikisha shughuli hiyo.
“Tunaweza kuzungumza jinsi tunavyotaka lakini tusipofuata sheria, hatutaenda mahali. Lazima tufuate sheria kuhakikisha kuwa mchakato wa kuwatimua magavana unasimama kwenye Seneti,” akasema Bw Kingi.
“Magavana nao wataendelea kuponyoka hata kama wamekosa. Hii ndiyo maana nimeitisha kikao na maspika wote wa mabunge ya kaunti ili tuzungumzie suala hili kwa ajili ya sheria kufuatwa wakati magavana wanatimuliwa,” akasema Bw Kingi.
Kiongozi huyo alionekana kuchemshwa na madai ya baadhi ya madiwani wa Isiolo kuwa Seneti ilikosea kwa kutofaulisha mchakato wa kumbandua Bw Guyo.
“Nahisi uchungu wenu lakini bila kufuata sheria magavana wataponyoka. Mtakuwa mkilaumu Seneti lakini kosa ni lenu kwa sababu hamkufuata sheria wakati wa kumwondoa gavana madarakani,” akaongeza.
Kung’ang’ania mabilioni ya pesa na magavana na siasa za urithi zimekuwa zikichangia nyingi za hoja za kuwaondoa magavana madarakani.
Magavana wengine nao pia wameondolewa madarakani na mahakama kutokana na mchakato wa kuwaondoa magavana madarakani kukosa kufuata sheria.
Seneti imeshughulikia zaidi ya hoja 20 za magavana kuondolewa mamlakani na mabunge ya seneti tangu utawala wa ugatuzi uanze mnamo 2013.
Maseneta James Murango (Kirinyaga), Edwin Sifuna (Nairobi) na Bonny Khalwale wa Kakamega nao wanasisitiza kuwa lazima mchakato wa kuondoa gavana ufuate sheria na lazima pia kuwe na ushahidi wa kutosha tena wa kuaminika.
“Mkifurusha gavana, huwa mmewapeleka kwenye baridi ya kisiasa kwa hivyo lazima ushahidi uwe mzito,” akasema Bw Murango.