Kinywa cha Kahiga chamchongea tena
KATIKA kipindi cha miezi minane pekee, Gavana wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga, amelazimika kujutia maneno yake ya kugawanya baada ya kukabiliwa na hasira ya umma.
Mnamo Februari, alitoa matamshi ya kuudhi kuhusu jamii ya Wamaasai akihudhuria mazishi Laikipia.
Sasa, amesherehekea kifo cha Waziri Mkuu wa pili wa nchi, Raila Odinga, aliyezikwa Jumapili iliyopita, pia akihudhuria mazishi.
Makosa hayo ya hivi punde yamekashifiwa vikali na kwa haraka, na baadhi ya viongozi wanaomtaka afunguliwe mashtaka.
Viongozi wa kisiasa wamesema kuwa mdomo wake unaeneza ukabila.
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kilichoongozwa na Odinga hadi alipofariki Oktoba 15 2025, kimesema Kahiga hafai kushikilia wadhifa katika utumishi wa umma.
Kama alivyofanya Februari, amelazimika kuomba msamaha ambao baadhi ya watu wameukataa.
Wakati huo huo, upinzani ulioungana, unaojumuisha pia chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa kisiasa wa Kahiga, unataka akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Wenzake katika Baraza la Magavana (CoG), na viongozi wa ODM Gavana Simba Arati (Kisii) na Bi Gladys Wanga (Homa Bay) wamesikitishwa na maneno yake wakati nchi bado inaomboleza kifo cha Raila.
Bi Wanga hasa alihusisha maneno ya Gavana Kahiga na Gachagua, akimlaumu kwa kueneza chuki na kutokuwa na heshima kwa Odinga, alipokuwa hai na sasa akiwa amekufa.
“Tunaka akamatwe mara moja na kufunguliwa mashtaka kwa maneno yake kuhusu kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga,” alisema Gavana Arati, akiongeza kuwa “maneno kama hayo yanalenga kugawanya Kenya.”
Akifahamu hasira iliyotokana na matamshi yake, Gavana Kahiga alijiuzulu haraka kama Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana.
Wito wa Gavana Arati wa Kahiga kukamatwa na kufikishwa mahakamani, unaungwa mkono na kifungu 62(1) cha Sheria ya Uwiano na Utengamano wa Kitaifa (NCI) ambacho kinatoa adhabu kwa anayeeneza maneno ya chuki, ubaguzi au nguvu dhidi ya mtu, kundi au jamii kwa msingi wa kabila au rangi.
“Kila mtu anayetoa maneno kwa nia ya kuchochea hisia za chuki, uhasama, vurugu au ubaguzi dhidi ya mtu, kundi au jamii yoyote kwa msingi wa kabila au rangi, anafanya kosa,” inasema sheria hiyo.
“Mtu kama huyo anaweza kuchukuliwa hatua na ikiwa atathibitishwa kuwa na hatia, atozwe faini isiyozidi Sh1 milioni au kifungo cha hadi miaka mitano au vyote pamoja.”
Katika video iliyosambaa mitandaoni, Gavana Kahiga, akizungumza katika lugha yake ya mama kwenye mazishi Oktoba 21 2025 katika eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri, aliitaka serikali ya Rais William Ruto na aliyefariki (akimaanisha Raila) kuwa wamepeleka rasilmali zote za Mlima Kenya katika maeneo ya Magharibi na Nyanza.
“Kwa majibu ya kilio kutoka Mlima Kenya, Mungu aliingilia kati akachukua maisha ya Raila. Sasa watu wameambiwa warudi kwenye ramani kwa sababu mpango ulikuwa ni kutufukuza. Lakini naye Mungu ni nani?
Je, anakula ugali nyumbani kwa mtu au kulala Kayole?” anaonekana akisema.
Aliongeza: “Mungu alikuja kwa njia yake mwenyewe. Alikuja kwa Baba (kumaanisha Raila) ili aweze kwenda na kusafisha mambo pale.”
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Gavana Kahiga, ambaye alisema maneno yake “hayakuwa ya kusherehekea,” kifo cha Raila, alibainisha kuwa ameamua kujiuzulu kama Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana kutokana na matamshi yake.
Hata hivyo, akiwa Kisumu Jumatano, Gavana Wanga aliongoza ujumbe wa viongozi wa chama kukosoa maneno ya Kahiga, akisema ni ya “kizamani na hayastahili kutolewa na mfanyakazi wa umma.”
“Ni upotovu kudharau mtu aliyekuwa mwanzilishi wa ugatuzi ambao umewezesha Kahiga kuwa gavana. Hata ofisi anayoshikilia ipo kwa sababu ya jitihada za Raila Odinga za marekebisho ya katiba. Kumcheka mtu aliyeweka uhuru wake hatarini kwa ajili ya demokrasia yetu ni aibu,” alisema Bi Wanga.
Upinzani ulioungana katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Dkt Mukhisa Kituyi, ulisema maneno ya Gavana Kahiga yanapaswa kulaaniwa na Wakenya wote kuanzia Kiongozi wa Chama cha UDA Rais William Ruto, Mwenyekiti Cecily Mbarire na Katibu Mkuu wa UDA Bw Hassan Omar.
“Hakika, UDA ya Rais Ruto inapaswa kutoa taarifa ya kumuonya Kahiga na kuomba umma msamaha kwa maneno yaliyoonekana kuwa yameandaliwa awali kuchochea vita vya kikabila,” alisema Dkt Kituyi.
Ripoti za Mercy Simiyu, Mercy Mwende na Domnic Ombok