Kisanga Ruto akirushiwa kiatu mkutanoni Migori
ZIARA ya Rais William Ruto katika Kaunti ya Migori Jumapili ilikumbwa na kisanga baada ya kiongozi wa nchi kupigwa na kiatu alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara huko Kuria Magharibi.
Kiatu kilionekana kikirushwa kutoka kwa umati na kumpiga Rais Ruto akiwa katikati ya hotuba yake.
Tukio hilo lilitokea wakati Kiongozi wa Taifa alipokuwa ziarani Migori kuzindua miradi ya serikali. Anatarajiwa kuwa katika eneo hilo kwa siku mbili hadi tatu.
Dkt Ruto awali alitembelea Suna Mashariki ambako alihudhuria ibada ya maombi ya madhehebu mbalimbali.
Baadaye alielekea Suna Magharibi na kuzindua ujenzi wa Chuo cha Kiufundi cha Piny Oyie kabla ya kufungua rasmi ofisi za kaunti ndogo.
Matukio yote haya yalifanyika bila vurugu na Rais aliwahutubia wakazi, akiwaeleza mipango ya serikali.
Alipofika Kuria, umati uliokuwa ukimsubiri ulikuwa mgumu kudhibiti. Wakati Dkt Ruto alipokuwa akizungumza, umati ulianza kusonga kuelekea jukwaani.
Katika hali hiyo ya taharuki, mtu ambaye hakutambuliwa mara moja alirusha kiatu kumpiga Rais.
Dkt Ruto alikuwa akifanya ishara kwa mikono wakati kiatu kilirushwa kuelekea usoni, lakini alifanikiwa kukizuia.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kiongozi wa Taifa alisema serikali inatekeleza ajenda ya maendeleo ya mageuzi itakayohakikisha hakuna sehemu ya nchi itakayosahaulika au kuachwa nyuma.
“Nilizindua rasmi mradi wa nyumba nafuu wa Kehancha wenye vyumba 298,” ilisema sehemu ya chapisho hilo lililoambatana na picha. Hata hivyo, wakati wa tukio hilo, video ya matangazo ilikatizwa kwa muda na muziki pekee ukawa unasikika.
Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Migori, Fatuma Mohamed, alisema tukio hilo lilitokea kwa sababu wakazi walikuwa na hamu ya kumuona rais wao na walitaka kuwa karibu naye.
“Hii inaonyesha kwamba watu hawa wanakupenda. Walitaka tu kuwa karibu nawe,” alisema.
Taifa Leo ilijaribu kupata maoni kutoka kwa maafisa wa usalama wa Migori lakini walisema hawakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo.
“Niliandamana na rais hadi Suna Mashariki na Magharibi,” alisema Kamanda wa Polisi Francis Nguli.