Habari za Kitaifa

Kitendawili cha aliko Gavana Orengo chazidi kuwa tata

Na KASSIM ADINASI, RUSHDIE OUDIA August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KITENDAWILI kuhusu kutoweka kwa Gavana wa Siaya, James Orengo, kwa wiki kadhaa kilizidi Jumatano Agosti 6, 2025, huku naibu wake William Oduol akikiri kuwa hana taarifa yoyote rasmi kuhusu alipo bosi wake kutoka kwa familia au Ofisi ya Gavana.

Wakati uo huo, Spika wa Bunge la Kaunti, George Okode, alikanusha uvumi kuwa Bw Orengo amejiuzulu, na kukataa madai kuwa anatelekeza majukumu ya ugavana.

Mara ya mwisho kwa Bw Orengo kuonekana hadharani ilikuwa mwezi Juni.

Bw Oduol, ambaye uhusiano wake na gavana Orengo umekuwa tete, alisema kuwa hajapokea taarifa yoyote rasmi kuhusu aliko Gavana kutoka kwa ofisi ya gavana au kwa familia.

Alielezea masikitiko makubwa kwa kile alichosema ni kushindwa kwa ofisi ya gavana kutoa taarifa rasmi, hali inayoacha mianya ya uvumi na taharuki miongoni mwa wakazi wa Siaya.

Kumekuwa pia na madai kwamba Spika Okode, huenda anatekeleza majukumu ya ugavana.

Bw Okode amekuwa akipokea wageni mashuhuri jukumu ambalo kwa kawaida hufanywa na gavana, naibu wake, au mawaziri wa kaunti.

Akizungumza na wanahabari mjini Kisumu, Bw Okode alisisitiza kuwa Bw Orengo bado ndiye kiongozi halali wa serikali ya kaunti ya Siaya na anaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida.

Tafsiri: BENSON MATHEKA