Habari za Kitaifa

Kitendawili cha vifo vya chokoraa 15 jijini Nairobi

Na DANIEL OGETTA January 30th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAJENEZA tisa madogo ya mbao yalifukiwa ardhini katika makaburi ya Lang’ata huku vijana wa mitaani, wengi bila viatu, wakishuhudia na kubaki na maswali kuhusu nini kinachowaua wenzao.

Baadhi walifuta machozi, wengine wakatazama tu kwa huzuni wakiaga marafiki waliokuwa kama familia kwao, waliokuwa wakigawana chakula kidogo na makazi ya karatasi jijini Nairobi.

“Ardhini ulitoka, na ardhini utarudi,” alisema mchungaji David Maina wa Kanisa la PEFA Lang’ata kabla ya kila mwili kuzikwa futi sita chini ya ardhi, makazi ya mwisho ya vijana hao.

Waliozikwa ni miongoni mwa watoto 15 wa mitaani waliokufa siku tofauti na ambao miili yao ilitolewa kutoka hifadhi ya Nairobi Funeral Home na Mochari ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki kwa mazishi ya pamoja yaliyoandaliwa na shirika la familia za mitaani.

Miili mingine sita imebaki katika mochari ikisubiri uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo.

Rekodi kutoka Nairobi Funeral Home zinaonyesha vifo vilitokea siku tofauti na sehemu tofauti za Jiji Kuu.

Rekodi zilizoonwa na Taifa Leo zinaonyesha wawili walikufa ghafla mnamo Desemba 26, 2025 katika mitaa ya Mlango Kubwa na Mathare, mwingine alijiua mtaani Kariobangi Desemba 29, 2025, huku wawili wengine wakifa kwa sababu za kiasili siku ya Krismasi na Boxing Day katika mitaa ya Pangani na Shauri Moyo.

Miongoni mwa waliokuwa na huzuni alikuwa Moses. Kwa utulivu, aliandika kuhusu rafiki yake Enock ambaye alisema hakuwahi kufikiria kuwa angekufa na kuzikwa haraka.

Alisema wakati mfupi waliokuwa pamoja na Enock utabaki kumbukumbu kwake. Hakuwahi kufikiria kuwa siku zake zingeisha haraka hivyo.

Hata hivyo, alisema hakumbuki mara ya mwisho walipoongea. Alisema, mara zote rafiki yake huyo alikuwa amelewa “kwa sababu kuishi mitaani kama chokoraa, huwezi kuwa mwangalifu”.

Enock na Moses walikuwa wakiongea mara kwa mara kuhusu maisha kwa jumla. Moses hakumjua sana Enock, isipokuwa hatima iliwaunganisha mtaani Mlango Kubwa kando ya barabara ya Juja.

“Nitakukosa, Enock,” alisema Moses akiwa na machozi.

Mary Nyambura alimfahamu Munyiri kama jirani mwema. Munyiri ni miongoni mwa watu tisa waliozikwa jana katika makaburi ya umma.

Kwa kutumia lugha ya mitaani, Nyambura alisema alikutana na Munyiri mtaani, na baada ya muda walijadiliana na kuwa marafiki. Walishirikiana na kuungana kwa muda, ingawa kwa muda mfupi.

Nyambura alisema walikuwa wakilala karibu na Pangani Girls High School.

Alisema rafiki yake Munyiri alikuwa mtu wa maneno machache. Lakini “siku moja tulimpata amekufa. Tunashuku alivamiwa na kisha kuuawa.”

Peter Wanjiru almaarufu Chokora Msafi, ambaye pia ni mratibu wa familia za mitaani, alisema wengi wa waliozikwa walikufa kati ya Novemba mwaka uliopita na mwaka huu.

“Sisi hatuko mitaani kwa hiari. Ni kwa sababu ya hali,” alisema Wanjiru.

“Sababu za vifo vya wengi ni baridi na njaa.”

Miili ya wengine wawili ilibaki Nairobi Funeral Home ambako saba ilichukuliwa jana kuzikwa.

Rekodi katika mochari zinaonyesha walikufa siku tofauti. Kwa mujibu wa wasimamizi wa makaburi, ada za mazishi mara nyingi hufutwa.

Lakini Agnes Kagure, ambaye shirika lake la Agnes Kagure Foundation liliandaa mazishi hayo, alisema walibeba gharama zinazotokana na “mazishi ya pamoja”.

“Wanakufa kwa utapiamlo. Wengine wanashambuliwa na wahalifu usiku. Wengine wanapata homa ya mapafu kwa sababu ya kulala katika baridi,” alieleza Bi Kagure.

“Tuliamua kutumia makaburi ya pamoja kwa sababu ni ghali kununua nafasi katika Makaburi ya Lang’ata.”

“Wengi wao wako kati ya miaka 18 hadi 35, pamoja na mtoto wa miezi mitatu. Hawa ndio watu ambao tungewapeleka katika taasisi za kiufundi ili wafunzwe shughuli za kiuchumi,” aliongeza.