Habari za Kitaifa

Kitendawili cha wanafunzi 122,908 wa CBC kutoweka ndani ya miaka mitatu

Na DAVID MUCHUNGUH, MERCY SIMIYU September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI 122,908 waliofanya mtihani wa Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA) wakiwa Darasa la 6 miaka mitatu iliyopita hawatafanya mtihani wa Gredi 9, Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) mwezi ujao, ikiwa ni pigo kubwa kwa sera ya serikali ya wanafunzi kujiunga na sekondari pevu kwa asilimia 100.

Mtihani wa KPSEA haukutumiwa kuwaweka wanafunzi katika shule za sekondari msingi kwa kuwa serikali ilikuwa makini kuhakikisha asilimia 100 katika kila hatua ya elimu, kulingana na mfumo wa elimu wa umilisi na utendaji (CBE).

Uamuzi huu ulifanyika kujaribu kukomesha kiwango kikubwa cha wanafunzi kuacha shule ambacho kimekuwa kikihusishwa na mfumo wa zamani wa 8-4-4, lakini inaonekana tatizo bado lipo.

Kulingana na takwimu ambazo Taifa Leo imeona, Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) limewasajili wanafunzi 1,130,699 kwa mtihani wa KJSEA wa 2025.

Hili ni darasa ambalo lilifanya mtihani wa KPSEA mwaka wa 2022, wakati wanafunzi 1,253,577 walishiriki wakiwa Gredi 6. Hii ina maana kuwa jumla ya wanafunzi 122,908 hawakufika Gredi 9 kwa sababu mbalimbali.

Huu utakuwa mtihani wa kwanza wa KJSEA kufanyika tangu mabadiliko kutoka kwa mfumo wa 8-4-4 hadi ule wa CBE.

Matokeo ya KJSEA yataamua ni shule gani za sekondari na mkondo wa taaluma wanafunzi wataelekezwa kulingana na utendaji wao na pia maslahi yao binafsi.

KNEC ilipofanya tathmini ya maendeleo ya wanafunzi mwaka wa 2019 darasa hili lilipokuwa Gredi ya 3, idadi kubwa zaidi ya wanafunzi 1,282,150 walishiriki.

Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema kuwa kupungua kwa idadi ya wanafunzi kutoka Gredi ya 6 mwaka wa 2022 hadi walioandikishwa kwa mtihani wa KJSEA mwaka wa 2025 kunatokana na sababu mbalimbali.

“Baadhi ya upungufu unatokana na sababu za kiasili kama vile vifo au kushindwa kuendelea na masomo. Wanafunzi wengine walichagua kujiunga na vyuo vya mafunzo ya kiufundi (VTCs). Wengine wamehamia mitaala mbadala kama vile shule za kimataifa. Pia kuna visa vya kuacha shule na kuchelewa kurudi shuleni, kwa mfano, kutokana na mimba za mapema au maradhi, lakini wana nafasi ya kurejea wakishapona,” aliambia Taifa Leo.

Waziri huyo alitetea sera ya asilimia 100, akisisitiza kuwa bado ipo imara licha ya hofu kuhusu maelfu ya wanafunzi wanaoonekana kutoweka katika mfumo wa elimu.

Alisema sera haipaswi kupimwa kwa wanafunzi wanaoshindwa kuendelea moja kwa moja hadi sekondari, bali kwa fursa nyingine zilizopo ndani ya sekta ya elimu.

“Sera ya asilimia 100 bado ipo. Kujiunga na VTC au mitaala mingine mbadala bado ni sehemu ya mfumo wa elimu. Wanafunzi wanaochelewa kama wasichana waliopata mimba, watarudi shule wakipata fursa,” alisema.

Kupotea kwa wanafunzi si tu kwa shule za msingi au bali pia sekondari. Kulingana na takwimu za usajili za KNEC, wanafunzi 996,078 wamesajiliwa kwa mtihani wa KCSE 2025.

Ikilinganishwa na wanafunzi 1,214,031 waliofanya mtihani wa KCPE Machi 2021 baada ya janga la Covid-19, hii inaonyesha kuwa wanafunzi 217,953 hawakufika mwisho wa shule ya upili.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA), Fuad Ali, alisema hakuwa na taarifa kuhusu takwimu hizo, akidai kuwa hazihusiani na eneo lake licha ya kuwa mwenyekiti wa kitaifa.

Hata hivyo, Chama cha Kitaifa cha Wazazi kilitoa wito wa kufanyika kwa ukaguzi wa haraka ili kubaini mahali watoto hao walipo na kueleza sababu ya kutoweka kwao bila maelezo.

Chama hicho kilitaja taarifa hizo kama pigo kubwa kwa sera ya asilimia 100, kikionyesha wasiwasi kuhusu hatima ya zaidi ya wanafunzi 340,000 wanaoonekana kupotea kwenye mfumo wa elimu wa Kenya licha ya ahadi ya serikali.

“Tunaitaka serikali ifanye uchunguzi na ukaguzi kamili. Baada ya kuangalia shule, lazima ibaini watoto hawa wako wapi. Serikali ilituahidi uhamisho wa asilimia 100, nasi tuliikubali ahadi hiyo. Sasa tunataka waseme waziwazi — watoto hawa wako wapi?” alisema mwenyekiti wa NPA Silas Obuhatsa.

Bw Obuhatsa alisema kuwa wakuu wa shule hutuma ripoti za kila siku kwa Wizara ya Elimu, lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu pengo hilo kubwa.