• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kitengo maalum chabuniwa DCI kufuatilia yanayoendelea mitandaoni

Kitengo maalum chabuniwa DCI kufuatilia yanayoendelea mitandaoni

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amesema wizara yake imebuni kitengo maalum katika Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) cha kuwafuatilia wanaotumia mitandao kuendeleza maovu.

Akiongea Jumatano katika Bunge la Seneti, Prof Kindiki pia alieleza kuwa kitengo hicho pia kitawalinda watu wanaopitisha jumbe mbalimbali katika mitandao dhidi ya kuandamwa.

“Ningependa kuthibitisha kuwa tuko kesi mbalimbali ambazo zimewasilishwa kwetu na watu au mabloga ambao wametishwa na watu fulani mitandaoni. Pia tuko na visa vingi ambapo watu fulani hutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kupitisha jumbe za kuchochea chuki. Kitengo maalum kimebuniwa katika DCI kushughulikia visa kama hivi,” Prof Kindiki akasema.

Waziri aliwaambia maseneta kwamba wizara yake itahakikisha kuwa Wakenya wanaotumia mitandao kujieleza kwa namna mbalimbali hawatishwi.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali kutoka kwa Seneta wa Meru Kathuri Murungi aliyetaka kujua hatua ambayo serikali imepiga katika uchunguzi kuhusu kifo cha mwanablogu wa kaunti hiyo aliyeuawa Daniel Muthiani almaarufu ‘Sniper’.

Akijibu, waziri huyo alieleza kuwa kando na washukiwa watano waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo, huenda watu wengine wakakamatwa hivi karibuni.

“Tunaamini kuwa ni uhalifu uliotekelezwa kwa njia ya kukanganya zaidi na huenda kuna washukiwa wengine wengi kando na watano waliokamatwa, ambao walihusika. Hata hivyo, tunaendelea kukusanya ushahidi wa moja kwa moja wa kuwahusisha watu wengine na mauaji hayo,” akaeleza.

Washukiwa watano ambao wanazuiliwa kuhusiana na mauaji ya Sniper ni Vincent Muriithi, Kenneth Murangiri, Christus Manyara Kiambi almaarufu Chris, Brian Mwenda almaarufu Brayo na Bonface Kithinji Njiiyia almaarufu Dj Kaboom.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki. PICHA | MAKTABA

Seneta Murungi alitaka kujua ni kwa nini wapelelezi wa mauaji hayo hawajawachunguza wadhamini wa washukiwa hao watano na kwa nini watu wengine hawajakamatwa kuhusiana na uhalifu huo.

Sniper alitoweka mnamo Desemba 2, 2023, na mwili wake ukapatikana umetupwa katika Mto Mutonga katika Kaunti ya Tharaka Nithi mnamo Desemba 16, 2023.

Waziri Kindiki alisema uchunguzi ulibaini kuwa mnamo Desemba 2, 2023, marehemu kabla ya mauti alikuwa nyumbani kwake alipopokea simu kutoka Bw Muriithi alitaka wakutane mahala fulani mjini Meru kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Gavana Kawira Mwangaza.

Mkutano huo ulitarajiwa kujadili tofauti kati ya Sniper na Gavana huyo, ili marehemu akome kumshambuliwa mkuu huyo wa kaunti ya Meru mitandaoni.

Alipofika, Prof Kindiki alieleza, mwanablogu huyo alikamatwa na kupelekwa katika Mto Mutonga katika eneo la Chakariga, kaunti ya Tharaka Nithi kabla ya kuuawa na maiti yake kutupwa mtoni.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wanne motoni kwa kuigiza wizi wa mkoba na kupakia...

Aibu wavuvi wawili wakiuawa kufuatia mzozo wa samaki

T L