Kithure Kindiki, hatimaye achukua nafasi ya Naibu Rais akiahidi kuwa mwaminifu kwa Rais Ruto
Naibu Rais Kithure Kindiki ameahidi kuwa mwaminifu kwa Rais William Ruto akitekeleza majukumu yake.
Katika hotuba yake jana Novemba 1, 2024 baada ya kuapishwa, Profesa Kindiki alisema amekuwa mwanafunzi mwema wa Rais Ruto na kwamba hatamwangusha katika majukumu mapya aliyompa ya kuwa msaidizi wake rasmi.
“Nimekuwa mwanafunzi wako mwema kwa miaka 20. Nimejifunza kuwa mnyenyekevu na mwaminifu, sitakuangusha katika majukumu mapya uliyonitwika,” akasema.
Prof Kindiki ameeleza kuwa angetaka kuhudumu kuhakikisha Kenya inapata mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kidemokrasia chini ya Rais William Ruto.
“Nitashirikiana na wenzangu serikalini, kuhakikisha kuwa nchi hii inasonga mbele,” akasema.
Amemshukuru Rais Ruto kwa kumwamini na kumtwika wadhifa huo mkubwa baada ya kumteua waziri wa usalama wa ndani aliohudumu kwa miaka miwili.
Prof Kindiki, aliapishwa Ijumaa katika hafla ya kufana iliyofanyika nje ya Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) iliyoshuhudiwa na Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome, miongoni mwa wageni mashuhuri.
Amechukua nafasi ya Rigathi Gachagua, ambaye alitimuliwa mamlakani na Bunge la Kitaifa mwezi Oktoba.