KNEC yaanza kusajili watahiniwa wa KPSEA, na haya ndiyo masharti
BARAZA la Kitaifa la Mtihani Kenya (Knec) limetangaza kuanza kwa usajili wa watahiniwa wa Gredi 6, kuanzia Januari 27 hadi Februari 28, 2025.
Watahiniwa wa Gredi 6 hufanya Tathmini ya Elimu ya Shule ya Msingi Kenya (KPSEA) mwishoni mwa shule ya msingi, kabla ya kujiunga na shule ya Sekondari Msingi.
Katika taarifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Knec David Njengere alisema kuwa watahiniwa lazima watimize vigezo vyote.
Alionya kuwa kusajili watahiniwa hewa ni kosa, jambo ambalo linaweza kusababisha kufutwa kwa usajili wa shule zinazohusika.
“Wanafunzi wote walio katika Gredi 6 watasajiliwa upya kwa tathmini hiyo kupitia tovuti ya usajili ya KPSEA ambayo itafikiwa kati ya Januari 27 na Februari 28 2025,” alisema.
Wanafunzi katika Gredi 6 wanahitajika kujiandikisha kwa KPSEA, tathmini iliyoundwa ili kutathmini umahiri wao kabla ya kujiunga na Sekondari Msingi.
Mchakato huo unahusisha kuthibitisha maelezo muhimu, ikiwa ni pamoja na majina, vyeti vya kuzaliwa na hati nyingine muhimu, ili kuhakikisha usahihi wa usajili.
“Marekebisho ya data ya wasifu wa mtahiniwa lazima yafanywe wakati wa usajili ili kuhakikisha usahihi wa habari zilizowasilishwa ikiwa ni pamoja na mpangilio sahihi wa majina ya wanafunzi kama yalivyoandikwa katika vyeti vyao vya kuzaliwa, jinsia, mwaka wa kuzaliwa, uraia, chaguo la elimu ya dini na wenye mahitaji maalum na walemavu,” alisema.
Dkt Njengere pia aliagiza uhamisho wa watahiniwa ukamilishwe kabla ya kufungwa kwa tovuti ya usajili mnamo Februari 28, 2025, ili kuhakikisha mchakato wa usajili unafanyika kwa uwazi.
“Hakuna uhamisho utakaoruhusiwa baadaye, zaidi mchakato wa uhamisho lazima ufanyike mtandaoni, ili kuepuka kurudiwa kwa watahiniwa,” alisema.
Zaidi ya hayo, alisema kuwa shule zilizo na watahiniwa chini ya watano hazitaruhusiwa kusajili watahiniwa wa KPSEA 2025 kama vituo huru.
“Shule zilizo na chini ya wanafunzi 5 hazitaruhusiwa kusajili watahiniwa wa KPSEA 2025 kama vituo huru vya kutathmini. Shule kama hizi zinashauriwa kuwasiliana na wakurugenzi wa elimu wa kaunti zao ili kutambua vituo vya kutathmini vya Knec vilivyo na zaidi ya watahiniwa 5 kwa usajili wa wanafunzi wao,” akasema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA