Knec yaonya kuhusu tathmini feki za matokeo ya KJSEA zinazoenezwa na shule
BARAZA la Kitaifa la Mtihani Kenya (KNEC) limeonya shule dhidi ya kupotosha umma kwa kuchapisha matokeo yasiyoidhinishwa na yasiyo sahihi ya mtihani wa Gredi ya Tisa (KJSEA).
KNEC imeshutumu baadhi ya shule kwa kujaribu kuchora taswira kwamba wao ndio walifanya vyema zaidi.
Knec inasema tabia hiyo inakiuka falsafa ya Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).
Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC Dkt David Njengere alisema kuwa CBE ina nia ya kukuza talanta ndiyo maana shule hazikupewa alama za wastani (mean aggregate).
Alisema kila somo linatahiniwa kwa njia tofauti na mafanikio yake kufuatiliwa badala ya alama kupewa uzingativu wa juu.
“Hakuna alama ya wastani ya shule jinsi ambavyo inaonyeshwa kwenye uchanganuzi feki unaoenezwa,” ikasema Knec katika mitandao yake ya kijamii.
“Umuhimu wa shule za sekondari msingi ni kuwasaidia wafahamu mtaala na kufahamu mchakato wa kujiunga na shule za sekondari za juu,” akaongeza Bw Njengere.
Alisema matokeo yaliyotolewa yalionyesha nguvu za mtahiniwa katika kila somo na hilo ndilo litatumika kama mwongozo wa kujiunga na Gredi ya 10.
Chini ya mtaala wa zamani wa 8-4-4, Knec ilikuwa ikitoa alama na jinsi shule zilivyofanya, hili likitumiwa kudhihirisha kuwa shule moja ilifanya vyema kuliko nyingine.
Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Wazazi Silas Obuhatsa aliwataka wazazi wafahamu mtaala na mfumo mpya wa elimu kisha wafuatilie mienendo ya watoto wao.