Habari za Kitaifa

Koome akohoa sasa

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

JAJI Mkuu Martha Koome sasa anamtaka mtu yeyote mwenye ushahidi kuwa majaji au maafisa fulani wa Idara ya Mahakama ni wafisadi auwasilishe kwa Tume ya Idara ya Mahakama (JSC) ili utaratibu wa kuwaadhibu kisheria uanzishwe.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jaji Koome, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa JSC, amewahakikishia Wakenya kuwa tume hiyo itashughulikia malalamishi au madai ya ufisadi kuhusu majaji “haraka na kwa mujibu wa Katiba”.

“JSC inayo rekodi ya kuchukua hatua dhidi ya afisa yeyote wa Idara ya Mahakama aliyepatikana na hatia ya kukiuka kanuni ya utendakazi na maadili au kushiriki ufisadi,” akasema.

Mfano wa hivi punde ni hatua ya tume hiyo kumtimua afisini aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Said Juma Chitembwe kwa tuhuma za ufisadi.

Hatua ya Bw Chitembwe kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo iligonga mwamba kuanzia hatua ya Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Juu.

Kauli ya Jaji Mkuu Koome imejiri Jumatatu siku moja baada ya Rais William Ruto kudai majaji huhongwa ili kutoa maagizo ya kusitisha utekelezaji wa mipango na miradi ya serikali yake.

“Tunaheshimu Idara ya Mahakama lakini ukiukaji wa sheria unaoendeshwa na majaji wafisadi sharti ukome nchini… au tutaukomesha kwa vyovyote vile,” Dkt Ruto akasema katika eneo la Njabini, Kaunti ya Nyandarua mnamo Jumanne.

Alikuwa amehudhuria mazishi ya babake Seneta wa Nyandarua John Methu, Mzee Michael Maigo.

Dkt Ruto aliapa kuwa miradi ya barabara katika eneo la Nyandarua iliyositishwa na agizo la mahakama itaendelea “wapende wasipende”.

Lakini Alhamisi Jaji Koome, bila kumtaja Rais kwa jina, alisema kuwa JSC imeghadhabishwa na kwamba majaji na maafisa wa  mahakama wamekosolewa hadharani na kukashifiwa kwa kutoa kutoa maagizo yanafasiriwa kupinga mipango na sera za sera.

“JSC ingependa kusisitiza uhuru na maadili ya idara ya mahakama kama tawi la serikali inavyoelezwa kwenye Katiba na tunatoa wito kwa majaji na maafisa wa idara ya mahakama kuendelea kutekeleza majukumu yao bila woga wala mapendeleo,” akaeleza.