Habari za Kitaifa

Koome kwa polisi: Wakabili madaktari wanaogoma

April 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

INSPEKTA Jenerali wa Polisi, IG Japhet Koome, Jumapili, Aprili 14, 2024, aliwaagiza makamanda wa polisi nchini kuwakabili vikali madaktari wanaogoma.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Bw Koome aliwaonya madaktari wanaogoma dhidi ya kuhujumu haki za raia wengine na kuvuruga shughuli za kawaida katika hospitali za umma.

“Kwa sababu za usalama wa kitaifa, Makamanda wote wa Polisi, wameagizwa kukabiliana na hali kama hizo kikamilifu na kulingana na sheria. Tungetaka kuwatahadharisha madaktari wote kujiepusha na vitendo vya kuhujumu haki za wengine wanapogoma. Hatutavumilia juhudi zao za kuvuruga shughuli za kawaida katika hospitali za umma,” akasema Bw Koome.

Alisema kuwa idara hiyo imeshuhudia na kupokea ripoti kuhusu matukio yasiyofaa yanayotokana na mgomo huo. Baadhi ya vitendo hivyo ni wahudumu wa afya kulala barabarani, hali inayoathiri shughuli za uchukuzi, uendeshaji magari na usafirishaji wa watu.

Kulingana na Bw Koome, madaktari hao wamekuwa wakivuruga shughuli za umma, kwa kupuliza firimbi na vuvuzela wakati wa maandamano yao.

Alisema ni hali ambayo imekuwa ikizua usumbufu mkubwa kwa wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini.

“Licha ya Katiba kuweka wazi kanuni na masharti yanayofaa kuzingatiwa na waandamanaji, madaktari wameendelea kukiuka kanuni hizo,” akasema.

Akaongeza: “Tuna habari kwamba kuna watu wasio wahudumu wa afya wanaolenga kuzua usumbufu kwa umma kwa kurai watu zaidi kujiunga na maandamano hayo. Hilo ni jambo linalohatarisha usalama wa umma.”

Wakati huo huo, Bw Koome aliwahakikishia Wakenya kwamba hali ya usalama nchini iko sawa na polisi wamejitolea kuudumisha.

Taarifa yake inajiri siku chache baada ya serikali kupiga marufuku miungano na maandamano ya madaktarti, ikiyataja kuwa kinyume cha sheria.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, alitaja mgomo huo kuwa ukiukaji wa agizo la mahakama.

Tayari, Rais William Ruto amesema kuwa serikali haina fedha za kutosha kulipa kiwango kinachoitishwa na madaktari.

Muungano wa madaktari nchini, kupitia Katibu Mkuu wake Dkt Davji Atellah, umeapa kuendeleza mgomo huo.