Habari za Kitaifa

Korti sasa tumaini pekee la Gachagua baada ya Seneti kumpiga teke la mwisho

Na ROSELYNE OBALA October 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Rigathi Gachagua huenda ataelekea mahakamani kuomba hatua ya kutimuliwa mamlakani na Seneti isitishwe kwa muda hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.

Bw Gachagua anaweza kuendeleza mapambano mahakamani walivyofanya magavana na kusalia afisini licha ya kuondolewa na Seneti.

Kwa mfano, licha ya aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora kutimuliwa na Seneti mara mbili; bado alikamilisha muhula wake wa kwanza hadi 2017.

Bw Wambora alishinda kwa mara nyingine katika uchaguzi wa mwaka huo. Naye Gavana wa Meru Kawira Mwangaza angali anahudumu licha ya kuondolewa afisini na Seneti baada ya mahakama kuingilia kati.

Duru zinasema kuwa Naibu Rais yu tayari kupambana hadi Mahakama ya Juu, mapambano ambayo huenda yakaendelea hadi mwishoni mwa muhula wake na Rais William Ruto.

Wakimtetea katika kesi kadhaa alizowasilisha mahakamani kujaribu kuzuia Bunge la Kitaifa na Seneti kushughulikia hoja hiyo iliyodhaminiwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, mawakili wa Bw Gachagua walitoa dalili kuwa watapambana hadi Mahakama ya Juu.

Mawakili hao wanalenga kukosoa shughuli ya ushirikishaji wa maoni ya umma kuhusu hoja hiyo kabla ya kujadiliwa na kupitishwa katika Bunge la Kitaifa Oktoba 8, mwaka huu.

Mawakili wa Bw Gachagua wanashikilia kuwa shughuli hiyo haikuendeshwa inavyopasa kisheria na kwamba Bunge la Kitaifa halikushirikisha majibu ya Naibu Rais.

Aidha, wanasema makosa ambayo Bw Gachagua ameelekezewa hayana msingi wowote na ushahidi uliowasilishwa si thabiti.

Naibu Rais mwenyewe amekuwa akishikilia kuwa walichaguliwa kwa tiketi moja na Rais William Ruto na hafai kutolewa afisini na wabunge wachache kwa misingi ya mashtaka ya kusingiziwa.

Katika Seneti, mawakili wa Bw Gachagua walikosoa ushahidi uliowasilishwa na mashahidi wa Bunge la Kitaifa, hali ambayo imempa Naibu Rais matumaini kuwa atakuwa na kesi thabiti mahakamani endapo seneti itamwondoa afisini.

“Tuna matumaini makubwa kwa Idara ya Mahakama. Mahakama zetu huendesha shughuli zake kwa kuzingatia haki na utaalamu na nina uhakika kwamba majaji wetu watalinda Katiba na utawala wa sheria. Aidha, watazingatia matakwa ya wananchi,” Bw Gachagua alisema Jumapili, Embu.

Ingawa mchakato huo ni wa kisiasa, ni wa kihistoria kwa kuwa unalenga kubaini ikiwa mashtaka yaliyowasilishwa na Bunge la Kitaifa yanatosha kuwezesha kuondolewa afisini kwa Naibu Rais.

Kulingana na kipengele cha 149, Rais atamteua naibu wake mpya ndani ya siku 14 baada ya kupitishwa kwa hoja hiyo katika Seneti. Kisha Bunge la Kitaifa litakuwa na muda wa siku 60 kuidhinisha au kumkataa mtu huyo.

Katika kupinga kuondolewa kwake afisini, Bw Gachagua atahitajika kuelekea mahakamani kuzuia kuchapishwa kwa tangazo la kumtimua afisini kwenye gazeti rasmi la serikali.

Tangazo hilo linatarajiwa kuchapishwa na Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi.