Habari za Kitaifa

Korti yafungulia Ruto milango ya kuteua jopo kuajiri makamishna wa IEBC

Na SAM KIPLAGAT, SIMON CIURI January 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeruhusu Bunge kuwasilisha majina ya walioteuliwa wanachama wa jopokazi la uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kwa Rais William Ruto.

Hii ni baada ya Jaji Dorah Chepkwony kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa mwaka jana, kupinga orodha hiyo kufuatia madai kuwa walemavu hawajajumuishwa katika jopokazi hilo.

Bw Boniface Njogu alihoji kwamba uteuzi haukuzingatia Vifungu 10 na 54(2) vya katiba vinavyohitaji angalau asilimia tano ya wanachama katika jopo wanapasa kuwa watu wanaoishi na ulemavu.

Jaji Chepkwony, hata hivyo, alipuuzilia mbali kesi hiyo akisema mlalamishi hakuthibitisha kuwepo kwa ukiukaji wa katiba na sheria katika uteuzi huo.

“Mlalamishi amewasilisha ushahidi usiotosha kuruhusu mchakato wa uteuzi kuchukuliwa kwamba umekiuka katiba,” alisema Jaji.

Uteuzi wa makamishna wa IEBC umekabiliwa na pandashuka chungu nzima ikiwemo migawanyiko ya kisiasa na changamoto tele za kisheria.

Kesi nyingine iliyowasilishwa na Dkt Augustus Kyalo Muli, inasubiri kusikizwa katika korti ya rufaa japo hakuna amri iliyotolewa kusimamisha jopokazi la uteuzi kuteuliwa rasmi.

Dkt Kyalo wa chama cha National Liberal Party alifika Mahakama ya Rufaa mwaka uliopita, baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Janet Mulwa, kutoa uamuzi kwamba hafai kuteuliwa kwa sababu chama chake hakina wawakilishi katika bunge la kitaifa.