Korti yamzima Ruto kuhusu uhamiaji eCitizen
MAHAKAMA Kuu imesitisha agizo alilotoa Rais William Ruto kwa mashirika 34 ya serikali kuhamia jukwaa la malipo ya eCitizen.
Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye, vilevile alitoa amri kuzuia kutimuliwa kwa wakurugenzi wa mashirika hayo kwa kukosa kuhamishia huduma zao eCitizen alivyoagiza Rais Ruto.
“Tukisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa Desemba 5, 2024, amri ya muda imetolewa kusitisha utekelezaji wa agizo lililotolewa Novemba 18, 2024 kulazimisha walalamishi 1-34 kuanzisha au kuhamia kwa jukwaa la eCitizen,” aliamuru Jaji.
Shirika la Kituo cha Sheria lilipinga agizo alilotoa Dkt Ruto, likilitaja kama lililotolewa ghafla pasipo utaratibu.
“Agizo hilo linahujumu kanuni za uongozi bora, uwazi na uwajibikaji jinsi zinavyoelezwa katika Katiba,” lilisema shirika hilo.
Katika hotuba yake Novemba 28, Rais Ruto alishutumu baadhi ya mashirika ya serikali kwa kutumia mbinu mbadala za malipo alizodai zinahujumu uwajibikaji na kuwezesha ufisadi.
Dkt Ruto kisha aliyapa mashirika hayo makataa ya wiki moja kuhakikisha huduma zote na malipo yanatekelezwa kupitia tovuti ya eCitizen.
Kituo Cha Sheria na Bw Hillary Mokaya katika kesi walihoji kuwa agizo hilo halina uwazi wala msingi kisheria na hivyo linahujumu hadhi ya utawala wa kisheria jinsi inavyohitajika kikatiba, ambayo ni muhimu kwa uongozi bora na kuvutia imani ya umma.
Agizo hilo, kulingana na Kituo Cha Sheria, linakiuka maadili na kanuni zinazohusu huduma ya umma, ikiwemo viwango vya juu vya maadili ya kitaaluma, utendakazi bora, matumizi mwafaka ya raslimali na uwajibikaji kwa vitendo vya kiusimamizi.
Korti iliagiza kesi hiyo kusikizwa Januari 31, 2025.
IMETAFSIRIWA NA MARY WANGARI