Korti yataka mashtaka ya Mackenzie yapunguzwe
NA BRIAN OCHARO
MAHAKAMA Kuu mjini Malindi imeamuru Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kupunguza mashtaka ya mauaji dhidi ya mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na washirika wake kutoka mashtaka 191 hadi 12 pekee.
Jaji Mugure Thande alikubaliana na Mackenzie na washirika wake 29 kwamba mashtaka yalikuwa mengi sana na yatasababisha kucheleweshwa kwa kesi hiyo bila sababu na kuwaathiri washtakiwa.
“ODPP inaagizwa kupunguza idadi ya mashtaka ya mauaji kutoka 191 hadi 12 pekee. Kupunguza idadi ya mashtaka kutarahisisha utoaji wa haki haraka kwa wahusika wote kando na kuokoa muda wa mahakama,” alisema Jaji.
Jaji Thande aliagiza kwamba marekebisho haya yafanywe ndani ya siku 21 na mashtaka mapya yaliyowasilishwa ndani ya muda huo.
Wakati huo huo, jaji huyo ameamua kuwa Mackenzie na wafuasi wake walishtakiwa ipasavyo kwa kuwa karatasi ya mashtaka haikuwa na dosari.
Jaji Thande alisema mashtaka yanayowakabili Mackenzie na washtakiwa mwenzake yaliandaliwa ipasavyo na washukiwa walishtakiwa kwa mujibu wa sheria.
“Shtaka hilo, kama lilivyowasilishwa halitawaadhiri Mackenzie na washtakiwa wenzake,” Jaji alisema.
Mackenzie na kundi lake walipinga mashtaka hayo, wakilalamikia idadi ya makosa ambayo wameshtakiwa nayo na kwamba karatasi ya mashtaka ilikuwa na dosari.
Hata hivyo, DPP aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo ikibainisha kuwa kila shtaka linaonyesha idadi ya watoto wanaodaiwa kuuawa na washtakiwa katika msitu wa Shakahola.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachomlazimisha DPP kupunguza idadi ya mashtaka ya mauaji dhidi ya Mackenzie na washtakiwa wenzake 29.
Washtakiwa wote 30 kwa pamoja walikana mashitaka 191 ya mauaji kinyume na sheria.
Inadaiwa walitenda makosa hayo tarehe isiyojulikana kati ya Januari 2021 na Septemba 2023 katika eneo la Shakahola, Kaunti Ndogo ya Malindi, Kilifi.
Mahakama imeambiwa kuwa baadhi ya watoto waliouawa walitambuliwa kwa majina yao huku wengine wakikosa majina kwa kuwa hawakutambuliwa na wapelelezi.
Mahakama pia iliambiwa jinsia za baadhi ya watoto waliouawa haikujulikana.
Kesi hiyo itatajwa Julai 2024.