Korti yatupa nje rufaa ya KDF katika kesi ya kurutu aliyebaguliwa kwa kuugua Ukimwi
JESHI la Ulinzi la Kenya (KDF) limepata pigo la kisheria baada ya Mahakama Kuu kuidhinisha uamuzi ulioipata jeshi na hatia ya kumbagua kijana aliyetaka kujiunga na jeshi kutokana na hali yake ya virusi vya Ukimwi, na pia kufanya uchunguzi wa kiafya bila hiari yake na ushauri unaotakikana kisheria.
Mahakama ilitupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Ulinzi na KDF, na hivyo kuthibitisha uamuzi wa Julai 2024 wa Baraza la Kusikiliza Masuala ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, lililompa mlalamishi, aliyetambuliwa kama PKJ, fidia ya Sh1 milioni.
Kesi hiyo ilitokana na tukio la Desemba 2021 ambapo Bw PKJ alidai kufanyiwa vipimo vya lazima vya virusi vya Ukimwi bila hiari wakati wa mchakato wa kusajili makurutu wa jeshi.
Hata baada ya kutangazwa kuwa yuko sawa kiafya na kupewa barua rasmi ya kuripoti katika Chuo cha Mafunzo ya Makurutu Eldoret, kijana huyo alisema alifukuzwa ghafla siku chache baada ya kuanza mafunzo.
Katika ushahidi wake, alieleza kuwa maafisa wa jeshi walitangaza hadharani hali yake ya Ukimwi mbele ya makurutu wenzake kwa njia ya kumdhalilisha, wakimwambia “aende kutafuta matibabu” badala ya kuendelea na mafunzo ya kijeshi.
Alisema hatua hiyo ilikiuka haki yake ya faragha, hadhi na utaratibu sahihi wa kiutawala, kinyume na sheria za Kenya za upimaji wa virusi vya Ukimwi.
Serikali ilidai kuwa baraza hilo halikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ikisema masuala yanayohusiana na ajira yanapaswa kushughulikiwa na Mahakama ya Ajira na Leba pekee.
Lakini jaji alisema kuwa kesi hiyo ilihusu uvunjaji wa Sheria ya Kuzuia na Kudhibiti Ukimwi, na wala si masharti ya ajira, hivyo iliwasilishwa kwa baraza kisheria.
Jaji alisisitiza kwamba kiini cha kesi hakikuwa ajira, bali “namna maafisa wa KDF walivyoshughulikia suala la hali ya Ukimwi ya mlalamishi.”
Alisema Baraza hilo lilikuwa na mamlaka kamili ya kusikiliza malalamishi hayo kulingana na sheria.
Mahakama pia ilitupilia mbali madai kuwa baraza hilo liliingilia jukumu la Bunge kwa kuagiza KDF kurekebisha kanuni na taratibu zake za usajili ndani ya siku 90.
“Ushahidi wa mlalamishi haujakosolewa. Alieleza kuwa alifukuzwa mafunzoni kwa sababu ya hali yake ya Ukimwi, na ushahidi huo umesalia bila kupingwa,” alisema jaji.
Mahakama ilisema kuwa KDF ilishindwa kutoa rekodi za usajili au mashahidi wa kupinga madai ya Bw PKJ.
Kwa upande wake, Bw PKJ aliwasilisha hati muhimu kama barua ya kujiunga na ripoti za uchunguzi wa afya, huku jeshi likishindwa kuwasilisha orodha ya makurutu au ushahidi mwingine ambao ungeweza kupinga madai hayo.
Mahakama ilisema kuwa jeshi halikuwasilisha ushahidi wa kitabibu au kitaalamu kuthibitisha kuwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi hawawezi kutekeleza majukumu ya kijeshi.
“Kama ushahidi huo ungewasilishwa, huenda uamuzi ungekuwa tofauti,” ilisema sehemu ya hukumu hiyo.
Ingawa KDF ilidai kuwa makurutu husaini fomu za kukubali kufanyiwa uchunguzi wa afya, mahakama ilisema hakuna ushahidi ulionyesha Bw PKJ aliruhusu kufanyiwa kipimo cha Ukimwi au kwamba alipata ushauri kabla na baada ya kipimo kama sheria inavyohitaji.
Mahakama ilishikilia kuwa kutofautisha watu kutokana na hali ya virusi vya Ukimwi ni ubaguzi usio na msingi wowote isipokuwa kuwe na sababu ya kitabibu.
“Hatua ya waajiri kubagua watu wasio na virusi vya Ukimwi dhidi ya wale walio na virusi hivyo ni kukiuka haki za msingi za Katiba,” alisema Jaji, akibainisha kuwa Bw PKJ hakuwahi kupewa sababu nyingine yoyote ya kufukuzwa ila hali yake ya Virusi vya Ukimwi.