• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Korti yatupa ombi la wakazi wa Kilifi waliotaka serikali isipewe chuo cha utalii cha Ronald Ngala

Korti yatupa ombi la wakazi wa Kilifi waliotaka serikali isipewe chuo cha utalii cha Ronald Ngala

MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali ombi la baadhi ya wakazi wa Kilifi ambao walitaka kusimamisha kwa muda kupeanwa kwa chuo cha utalii cha Ronald Ngala kwa serikali kufunguliwa rasmi au kuanzisha operesheni zake.

Wakazi hao walikuwa wanataka kusimamishwa kupeanwa kwa mradi huo kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi ambayo waliwasilisha itakayo maagizo mojawapo likiwa washtakiwa walikiuka sheria kwa kukosa kuweka wazi fedha za umma zilizopeanwa kwa ujenzi wa chuo hicho.

Jaji Stephen Githinji, akiwa Malindi alisema kuwa waliowasilisha kesi hawakuwa wameonyesha kesi kuwa ya kubishaniwa ambayo inataka maagizo waliokuwa wanataka kupewa.

Jaji Githinji alisema kuwa hata katika ombi hilo la kuzuia linalonuia kusimamisha kuzinduliwa kwa chuo hicho, inaweza kusemekana ya kuwa mradi huo umefika hatua za kumalizika.

Aliongeza kusema kuwa kusimamisha kupeanwa au kuzinduliwa kwa mradi huo hautasuluhisha masuala ya utatata na itakuwa si kwa maslahi ya umma na faida kwa mradi huo.

“Kwa njia yeyote, usawa wa urahisi unapendelea washtakiwa ikizingatiwa jamii inafaa kufaidika,” alisema Jaji Githinji.

Waweka kesi ni Raymond Chonga, Amani Mkenya, Ali Said, Riziki Shikani, Zani Juma, Furaha Kahindi, Salim Zablon, Miriam Mishi, David Mbero, Emmanuel Mzungu na Moses Katana.

Wameshtaki kampuni ya ujenzi ya Mulji Devraj & Brother, Board of Trustees of the Architects Ltd, Tourism Fund, Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Spika wa Bunge la Kitaifa, Kamati ya ukaguzi wa uekezaji ya bunge la kitaifa (PIC) na Mwanasheria Mkuu.

Jaji Githinji alisema kuwa kutokana na hati ya kiapo ya Bw Chonga, kizuizi ambacho waweka kesi walikuwa wanakitaka, msingi wake ni madai ya mchakato usiokuwa sawa wa ununuzi, ufadhili na utekelezwaji wa mradi huo wa Utalii.

Pia alisema kuwa kesi ya walalamishi ilikuwa ni kwamba bajeti ilibadilishwa hadi Sh8.9 bilioni kutoka Sh1.95 bilioni na kwamba hakukuwa na uwazi katika mchakato wote mzima.

“Maagizo yanayoombwa na walalamishi kwa maoni yangu yakipeanwa yanaweza kumaliza kesi nzima mapema.Pesa tayari zishatumika katika mradi na kutokana na kukiri kwa Bw Chonga,maendeleo kadhaa yamefanywa katika mradi,” alisema jaji Githinji.

Katika ombi lao, walalamishi walisema kuwa tangu kupeanwa kwa zabuni hiyo, kumekuwa na mabadiliko kadhaa ambayo yamefungua nafasi ya kufuja pesa za umma.

Walalamishi hao pia walisema kuwa washtakiwa walikuwa wanabadilisha fedha za mradi huo bila kushauriana au kukubaliwa na baraza la mawaziri vile inahitajika katika miradi hiyo.

Waliongeza kusema kuwa wanaanchi watapata hasara kubwa iwapo mradi huo utazinduliwa rasmi kabla ya fedha za umma kuhesabiwa vizuri.

Mahakama pia ilitupilia mbali ombi la kupinga lilokuwa limewasilishwa na kampuni ya Mulji Devraj kwa kukosa msingi wowote.

Kampuni hiyo ilikuwa inasema kuwa walalamishi hawakuwa na uwezo au haki ya kufika mahakamani na kuendelea na kesi dhidi yao (kampuni). Kesi itatajwa Aprili 9, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Putin kifua mbele uchaguzi ukinukia

Alikiba afungua kituo cha redio na televisheni

T L