KPC kulipa fidia ya Sh3b kwa walioathirwa na mafuta
MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi Ijumaa iliamuru Kampuni ya Kusambaza Mafuta ya Kenya (KPC) iwalipe wakazi 3,075 wa eneo la Thange waliothibitishwa kuathirika na uvujaji wa mafuta kwenye bonde la Mto Thange miaka 10 iliyopita, fidia ya Sh3 bilioni.
Majaji watatu Christine Ochieng, Theresa Murigi na Annette Nyukuri pia waliamuru KPC kulipa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) Sh900 milioni kusaidia kurejesha mazingira kwenye bonde hilo lililochafuliwa na mafuta.
Majaji hao walikubaliana na walalamishi kwamba mashirika ya KPC na NEMA yalikiuka haki zao za kikatiba kama wakazi, zikiwemo haki ya mazingira safi na salama, haki ya maisha, utu na upatikanaji wa taarifa, kufuatia tukio la uvujaji wa mafuta mwaka wa 2015 ambalo liliathiri vyanzo vya maji.
KPC ililaumu tukio hilo kwa bomba la mafuta lililochakaa, lakini majaji walieleza kuwa wakazi wa Thange walikuwa wamearifu kampuni kuhusu kutu kwenye bomba hilo miaka mitano kabla ya tukio, lakini hakuna hatua ambazo KPC na NEMA zilichukua kuzuia janga hilo la kimazingira.
“Wajibu wa kikatiba wa kulinda mazingira ulipuuzwa na wahusika,” alisema Jaji Murigi. Mahakama ilisema kuwa KPC tayari ilidai kuwa imelipa Sh38 milioni kwa familia 342 zilizoathiriwa, lakini iligunduliwa kuwa vocha za malipo zilitolewa bila taarifa ya kutosha kwa waathiriwa, hivyo hazikuwa halali.
“Vocha hizo ni kinyume cha Katiba, hazina uhalali wowote na zinabatilishwa. KPC inaagizwa kuwalipa walalamishi Sh3,800,831,676 kama fidia mbalimbali ndani ya siku 120 kuanzia tarehe ya hukumu hii,” alisema Jaji Ochieng.
Majaji waliagiza KPC irejeshe mazingira ya Thange ndani ya siku 120, ikijumuisha ardhi, maji ya chini na juu, viumbe hai na eneo lote la mto kwa hali yake ya awali, na kuwasilisha ripoti mahakamani.

Nje ya mahakama, wakazi walishangilia kwa nyimbo na ngoma wakisherehekea ushindi huo.“Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, hatimaye haki imetendeka,” alisema mlalamishi mkuu Bw Muindi Kimeu. “
Huu ni ushindi mkubwa kwa watu wa Thange, taifa na mazingira,” alisema wakili wao Bw Kamau Muthanwa.Seneta wa Makueni, Bw Daniel Maanzo aliyekuwa mahakamani alisema hukumu hiyo imeongeza matumaini ya haki kwa kundi lingine la wakazi waliowasilisha kesi nyingine.