Habari za Kitaifa

Krismasi kavu kwa walimu wa JS walioteswa na mshahara duni mwaka mzima

Na WINNIE ATIENO December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imeongeza kandarasi za mafunzo za walimu 20,000 wa Sekondari Msingi (JS) kwa muda wa miezi 12 zaidi, hatua ambayo imezua hisia kali, ghadhabu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa maelfu ya walimu hao vibarua waliokuwa na matumaini ya kuajiriwa kuwa walimu wa kudumu wenye kulipwa pensheni kuanzia Januari 2026.

Uamuzi huo, uliotokana na agizo la moja kwa moja la Rais William Ruto, umetajwa na wadadisi wa masuala ya elimu kama pigo kubwa kwa walimu hao, ambao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kuhusu malipo ya chini, ukosefu wa marupurupu na hali ngumu ya kazi.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Bi Eveleen Mitei, alithibitisha kuwa, walimu wote 20,000 wa JS wataendelea kuhudumu katika vituo walivyo sasa kuanzia Januari 1, 2026 hadi Disemba 31, 2026 ili kukamilisha kipindi cha lazima cha miaka miwili cha mafunzo.

Bi Mitei alisema nyongeza hiyo inatokana na Sera na Mwongozo wa Walimu Wakufunzi 2019 na inalenga kuhakikisha hakuna upungufu wa walimu utakaosababisha kukwama kwa shughuli za kufunza katika shule za msingi zinazoendelea kutekeleza mtaala wa Elimu ya Umilisi CBE).

“Walimu hawa ni muhimu sana katika kuhakikisha mpito mzuri wa wanafunzi wa Sekondari Msingi. Kwa hivyo, kuongezwa kwa kandarasi zao ni hatua ya kuhakikisha hakuna pengo katika utoaji wa elimu,” alisema Bi Mitei.

Rais Ruto, ambaye amekuwa akitetea vikali mpango wa walimu vibarua, alisema serikali haina uwezo wa kuwaajiri kwa wingi mara moja kutokana na uhaba wa rasilmali na mzigo wa mishahara ya walimu unaoendelea kuongezeka.

“Hatuwezi kuajiri walimu 50,000 au 100,000 mara moja. Lazima tuwe na mpango unaofanya kazi. Ndiyo sababu tutawaajiri wote baada yao kuhudumu miaka miwili kama vibarua, hilo ndilo suluhisho la kudumu,” Rais Ruto alinukuliwa akisema mwezi uliopita.

Hata hivyo, TSC sasa inawataka walimu wote kusaini upya kandarasi zao ili kuthibitisha kama wanakubali kuendelea au la. Wale wanaokubali lazima pia wawasilishe bima ya binafsi ya ajali kwa kipindi kipya cha mwaka mmoja.

Kwa wale watakaokataa, nafasi zao zitajazwa moja kwa moja kutoka kwa orodha za waliokuwa tayari kwenye hifadhi data ya TSC katika kila kaunti.

Kwa mujibu wa taarifa ya TSC, maagizo yametumwa kwa wakurugenzi wa kaunti kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kabla ya Januari 23, 2026.

Lakini uamuzi huo haukupokelewa vyema na chama cha Walimu wa Sekondari Msingi (Kejusta). Mwenyekiti wake, James Odhiambo, alisema walimu wamedungwa “kisu moyoni” na serikali na sasa wako tayari kuchukua hatua kali.

“Huu sio uongozi. Watu wamefanya kazi kwa mwaka mzima bila marupurupu, bila mishahara ya kutosha, bila usalama wa kazi. Walitarajia barua za ajira ya kudumu kama zawadi ya Krismasi, lakini badala yake wanapewa mateso kwa mwaka mwingine,” Odhiambo alisema huku akionya kuwa, mgomo wa kitaifa unakaribia.

Kulingana naye, walimu wengi wamedhoofika kisaikolojia, hawajui mustakabali wao, na wengi wanahisi “kuvunjika moyo, kudharauliwa na kusalitiwa” na serikali waliyotegemea kuwatetea.

Kwa sasa, mwalimu vibarua wa JS hulipwa takriban Sh20,000 kabla ya makato, kiasi ambacho walimu wanasema “hakitoshi hata chakula na kodi.”

Baadhi yao wamekuwa wakilalamika kwamba, wanalazimishwa kufanya kazi ya walimu wa kudumu, ikiwemo kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi, kutayarisha mitihani, kutoa tathmini na kuripoti, lakini wanapokea malipo ya chini kuliko walimu walio kwenye ajira ya kudumu.

“TSC imeamua kuendelea kutuchukulia kama vijana wa kusaidia serikali. Hatuwezi kuendelea hivi,” alisema mwalimu mmoja kutoka Homa Bay.

Hofu sasa ni kwamba, ikiwa kundi kubwa la walimu wa JS litakataa kusaini kandarasi hizo, shule zitakosa walimu kuanzia Januari, na hivyo kusababisha mgogoro wa kitaifa wa kielimu katika darasa la JS ambalo tayari limekuwa na changamoto nyingi tangu lianzishwe.

Kando na vitisho vya mgomo, wazazi pia wameanza kueleza wasiwasi wao, wakisema mpango wa serikali wa kutatua changamoto za elimu unahitaji ukaguzi upya.

Hata hivyo, TSC imeapa kutekeleza nyongeza ya kandarasi bila mabadiliko yoyote, huku serikali ikishikilia msimamo mkali kwamba, wale watakaokataa mkataba watatimuliwa na nafasi zao kukabidhiwa wengine.