Habari za Kitaifa

Krismasi: Utalipa nauli ya juu, wamiliki wa Matatu wasema

Na KEVIN CHERUIYOT December 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA wanaopanga kusafiri kutoka maeneo ya mijini kuelekea mashambani kwa sherehe za Krismasi wameshauriwa kuwa tayari kulipa nauli za juu.

Ushauri huu umetolewa na Muungano wa Wamiliki wa Matatu (MOA), unaosimamia idadi kubwa ya magari ya uchukuzi wa abiria katika sekta hiyo nchini.

Mwenyekiti wa muungano huo, Albert Karakacha jana alisema kupunguzwa kwa bei ya petroli na dizeli wiki jana hakutachangia kushushwa kwa nauli.

Kulingana na bei mpya iliyotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (Epra) Jumamosi wiki jana, bei ya petroli ilishuka kwa Sh4.37 kwa lita huku bei ya dizeli ikipunguzwa kwa Sh3 kwa lita.

Alhamisi, Bw Karakacha alisema gharama ya kuendesha biashara ya matatu imeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya vipuri na mahitaji mengine ya kimsingi.