• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:55 AM
Kuchelewa kwa M-Pesa kwawaweka wengi hatarini kuchonga viazi

Kuchelewa kwa M-Pesa kwawaweka wengi hatarini kuchonga viazi

NA MWANDISHI WETU

SAFARICOM imesema inarekebisha hitilafu ya kiteknolojia inayochelewesha mchakato wa wateja kutuma, kupokea na kufanya malipo kupitia huduma ya M-Pesa.

Wateja waliojaribu kutumia huduma hiyo wameambiwa kuna mchakato wa uboreshaji huduma unaoendelea.

“Huduma ya M-Pesa inafanyiwa maboresho yaliyoratibiwa,” huu ndio ujumbe ambao wateja wengi wamepokea.

Ujumbe mwingine ambao watumiaji wamepatana nao ni ule unaowataka wasubiri kwa angalau dakika 10.

“Huduma ya M-Pesa inasita kidogo, hivyo haiwezi kukamilika inavyotarajiwa. Tafadhali jaribu tena baada ya dakika 10,” ujumbe huo umesema.

Kuchelewa kwa M-Pesa kunawaweka wengi katika hatari ya “kuchonga viazi”.

Msemo ‘kuchonga viazi’ unatumika kumaanisha kwamba mtu ameshindwa kulipa bili hotelini na hivyo basi hana budi isipokuwa kutumwa jikoni kuondoa maganda kwa viazi kama njia mojawapo ya kulipia mlo.

Wachangiaji kadhaa mtandaoni wametoa maoni yao kuhusu hali hiyo, wengi wakionyesha kukerwa mno.

Mchangiaji katika mtandao wa Facebook anayefahamika kama Devis Chirchir amesema anadaiwa Sh250 na mmiliki wa hoteli mojawapo nchini.

“Sasa nioshe vyombo kwa hii hoteli juu nadaiwa Sh250 (kwa mlo ambao) nimekula…,” ameandika Chirchir.

Naye Nyantika Dismas amesema hitilafu hiyo imeendelea kwa muda mrefu mno.

“Wamefanya makosa bila notisi, tutalipa bili aje sasa kutoka saa tano asubuhi hadi inakaribia saa saba mchana,” akalalama Dismas.

  • Tags

You can share this post!

2027: Mawaziri watumia kandanda kujipanga?

Gachagua akamilisha mbio za mita 100 licha ya kujikwaa

T L