• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Kupaa na kuporomoka kwa mwanahabari Jacque Maribe

Kupaa na kuporomoka kwa mwanahabari Jacque Maribe

NA ELIZABETH NGIGI

JACQUE Maribe aliwahi kupaa na kufikia viwango vya kutamaniwa na wengi, kabla tukio moja kubadilisha kabisa mkondo wa maisha yake na taaluma yake.

Maribe, 35, aliibuka kama mwanahabari mtajika, akizuzua wengi kwa ukwasi wake wa kitaaluma na uwezo wa kusisimua watazamaji. Alikuwa akiishi katika mtaa wa Buruburu, Eastlands viungani mwa jiji la Nairobi.

Maribe ambaye Ijumaa, Februari 9, 2024 aliondolewa mashtaka ya kumuua mfanyabiashara Monicah Kimani, alisomea Shule ya hadhi ya State House Girls.  Alianza safari yake ya tasnia ya utangazaji kwenye runinga ya K24 mnamo 2009 baada ya kufuzu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Aliendelea kunoa makali yake kama ripota wa masuala ya kisiasa katika runinga ya Kiss  kutoka 2011 hadi 2012 kabla ya kujiunga na runinga ya Citizen TV mnamo 2012.

Ni katika runinga ya Citizen ndipo alikwea ngazi na kuwa kipenzi cha wengi kutokana na sifa zake za utangazaji.

Nuru ilizidi kumwaangazia baada ya kuchukua usukani wa kutangaza taarifa za saa tatu usiku kwenye runinga ya Citizen pamoja na Waihiga Mwaura ambaye kwa sasa ni mwanahabari wa BBC.

Kando na hayo pia alikuwa ripota wa habari za siasa ambapo alikuwa akiripoti yanayojiri katika mikutano iliyohutubiwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijamii.

Ufanisi huo wote hata hivyo, uliingia doa baada yake kugonga vichwa vya habari kutokana na mauaji ya Bi Kimani mnamo Julai 2019. Hilo lilimlazimu ajiuzulu kutoka runinga ya Citizen.

Kati ya wanahabari wa kwanza kumhoji aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta

Alifanikiwa kupata nafasi ya kupanga mahojiano na Bw Kenyatta baada ya uchaguzi mkuu wa 2013 na mahojiano hayo yalifanyika mnamo 2014.

Alifanya mahojiano hayo akiwa mjamzito na yalikuwa ya kwanza kufanywa na Rais baada yake kuingia mamlakani mnamo 2013.

Aliwahi kudai kuwa mabosi wa runinga ya Citizen walimtaka Hussein Mohamed (sasa anahudumu katika ikulu) ila Rais Kenyatta akakataa na kusisitiza kuwa ni Maribe ndiye angeifanya.

“Nilipoenda kumwambia bosi kuwa nilipata mahojiano na Uhuru alishangaa na kuniuliza iwapo ningefanya kazi hiyo kwenye hali yangu ya ujauzito,”

“Nilikasirika na kumwaambia Rais Kenyatta kuwa usimamizi ulikuwa umeamua kumpa Hussein nafasi hiyo na akakataa. Alisema kuwa kama si mimi ningefanya mahojiano yenyewe, basi hayangefanyika,” akasema Maribe.

Wakati wa mahojiano hayo Rais Kenyatta alimtembeza Maribe ndani ya ikulu. Bado akiwa Citizen, Maribe alikuwa kati ya wanahabari ambao walikuwa wakitumia ndege za helikopta wakati wa kampeni za Jubilee mnamo 2017 Rais Kenyatta alipokuwa akisaka kuchaguliwa kwa mara ya pili.

Mnamo 2018, Maribe  alikuwa kati ya waliopokea Tuzo ya Rais  (HSC) ambayo iliwasilishwa kwake na Rais Uhuru Kenyatta. Maribe alikuwa na marafiki wengi baadhi wakiwa wanasiasa wakuu nchini.

Jinsi umaarufu na uanahabari wake ulivyoshuka

Safari ya ufanisi wa Maribe ilibadilika ghafla siku moja mnamo Septemba 2018.

Kupatikana kwa mwili wa mfanyabiashara Monicah Kimani katika makazi yake Nairobi kulitetemesha taifa na kushangaza wengi baada ya jina la Maribe kutajwa kuhusika.

Alikamatwa na mpenzi wake wakati huo Joseph Irungu maarufu kama Jowie kuhusiana na kuuawa kwa Kimani, 28.

Maribe akiwa na umri wa miaka 30 wakati huo alijipata pabaya zaidi baada ya kufungwa katika Gereza la wanawake la Lang’ata kwa siku 17 akipambana na kesi ya mauaji.

“Mambo yalikuwa yakiendelea vyema hadi tukio la siku moja, likavuruga kila kitu. Mambo yalibadilika tangu wakati huo,” akasema kwenye mahojiano na jarida la True Love.

  • Tags

You can share this post!

Jacque Maribe afutiwa kosa la kumuua Monicah Kimani

Jinsi Khalwale alivyotegua kitendawili cha familia pana

T L