Kurutu aliyefurushwa KDF kwa kuugua ukimwi ashinda kesi
MAHAKAMA Kuu imeamrisha jeshi lichapishe mwongozo wake wa usajili wa makurutu na kuamrisha kurutu ambaye alifuzu lakini akakosa kuingizwa jeshini arejeshwe kwenye idara hiyo ya ulinzi.
Mwanaume huyo alifuzu mafunzo ya kijeshi na kupita viwango vyote lakini akaondolewa baada ya vipimo vya kimatibabu kuonyesha alikuwa na virusi vya HIV.
Alienda mahakamani kupinga kuondolewa kwake akisema ni hatua ya kibaguzi kwa msingi wa afya.
Jaji Maureen Onyango alikubaliana na naye alikisema haki yake ilikiukwa ilhali katiba inamakinika usawa na heshima kwa haki ya yeyote kwa msingi wowote ule.
“Kuondolewa kwa kurutu huyo kulionyesha ubaguzi wa wazi na hauna msingi kabisa,” akasema Jaji Onyango.
Ameitaka jeshi nchini (KDF) ndani ya siku 90 ichapishwe mwongozo wa jinsi ambayo inashughulikia wanaoingia jeshini na wanaugua ukimwi.
Pia jaji huyo alimtaka Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya na Mkuu wa majeshi Meja Jenerali Charles Kahariri wafike kortini wenyewe ndani ya miezi minne kuthibitishia mahakama kuwa amri yake imetiliwa manani hasa kuhusu mwongozo huo.
Kurutu huyo aliwasilisha kesi akisimulia kuwa alijiunga na Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) mnamo 2018 na akafanya kazi kwa miaka mitano chini ya mpango wa Kazi Mtaani.
Mnamo 2021, Wizara ya Ulinzi ilitangaza nafasi za makurutu wa kujiunga na KDF.
Alituma maombi na kufuzu kwa usajili wa makurutu kwenye makao makuu ya NYS Ruaraka mnamo Novemba 24, 2021.
Alipimwa na akafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na kwa kweli ikathibitishwa yuko sawa kiafya.
Siku mbili baadaye alipokea barua kutoka KDF iliyompongeza kwa kufaulu na sasa angejiunga na KDF. Alitakiwa kujiunga na Chuo cha makurutu cha Eldoret mnamo Disemba 25, 2021 kupitishwa tena kwenye mchakato wa matibabu na kuanza mazoezi rasmi.
Baadaye alipatikana alikuwa akiugua ukimwi na mnamo Januari 2, 2022 alitimuliwa jeshini.
Mwanaume huyo aliambia korti kuwa afisa aliyesimamia usajili wa makurutu alitangaza hadharani kuwa alikuwa akiugua ukimwi na akamsindikiza hadi nje ya lango la chuo cha mafunzo ya Makurutu Eldoret.
Aliwashtaki Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Baraza la Ulinzi kwa kumbagua kwa msingi wa afya.