Habari za Kitaifa

KUUAWA KWA WAKILI: Bodaboda zimekuwa maficho ya majambazi?

Na WAANDISHI WETU September 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KUUAWA kwa kupigwa risasi kwa wakili mashuhuri, mhadhiri na mchapishaji wa vitabu vya sheria Mathew Kyalo Mbobu jijini Nairobi usiku wa Jumanne kumefufua kumbukumbu za visa sawa na hivyo nchini ambapo watu wamekuwa wakiuawa na kuporwa na watu wanaotumia pikipiki.

Mbobu alipigwa risasi na kuuawa katika Barabara ya Magadi, karibu na Chuo Kikuu cha Catholic, katika tukio ambalo limeishtua nchi, huku swali kuu likibaki ni nani aliyetaka mhadhiri huyo auawe.

Alishambuliwa na mtu aliyekuwa abiria kwenye pikipiki iliyotoroka na hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo ya kinyama.

Polisi walikaa kimya kwa zaidi ya saa 15 bila kutoa taarifa kuhusu kilichotokea, lakini baadaye walitoa taarifa wakisema maafisa wa upelelezi tayari walikuwa wakichunguza kisa hicho.

“Tungependa kuarifu umma kuwa mara tu tukio hilo liliporipotiwa, eneo la tukio lilitembelewa na kikosi cha maafisa wa upelelezi chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) wa Mkoa wa Kaunti ya Nairobi, Bw Benson Kasyoki,” ilisoma taarifa ya DCI.

Katika taarifa hiyo, DCI ilieleza kuwa imejitolea kuhakikisha wahusika wa kitendo hicho cha kikatili wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Vilevile, waliomba mtu yeyote mwenye taarifa yoyote itakayosaidia katika uchunguzi awasiliane na polisi.

Kifo kingine cha hivi karibuni kilichohusishwa na watu waliotumia boda boda ni cha Charles Ong’ondo Were, aliyekuwa Mbunge wa Kasipul, Kaunti ya Homa Bay.

Kama ilivyokuwa kwa Mbobu, Ong’ondo aliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa wakiendesha pikipiki katika Barabara ya Ngong.

Hata hivyo, washukiwa walikamatwa siku chache baadaye na maafisa wa DCI. Waliohusishwa ni Isaac Kuria Chege almaarufu Kush, na Allan Omondi Ogola. Polisi wanaamini kuwa Chege ndiye aliyefyatua risasi iliyokatiza maisha ya mwanasiasa huyo.

Chege amehusishwa na matukio kadhaa ya uhalifu jijini na alikuwa akitumia pikipiki wakati akitekeleza uhalifu huo.

Duru kutoka DCI zilimhusisha na matukio ya uhalifu hasa maeneo ya Eastlands, Dandora na Mwihoko.

“Alikuwa akijihusisha na uhalifu katika maeneo haya na alikuwa akifuatiliwa na polisi kwa miaka kadhaa. Aliwahi kuongoza tukio la unyang’anyi eneo la Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, na akafanikiwa kutoroka. Hata hivyo, mshirika wake aliuawa siku hiyo hiyo walipokuwa wakielekea Dandora,” duru hizo za polisi zilisema. Mshukiwa huyo kwa sasa amezuiliwa rumande huku kesi ikiendelea.

Mnamo Machi 2021, Jennifer Wambua alitekwa nyara na baadaye kuuawa. Kabla ya kifo chake, alikuwa akifanya kazi katika Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Uchunguzi ulionyesha alitolewa ofisini na mwanaume kabla ya mwili wake kupatikana siku kadhaa baadaye katika kichaka eneo la Ngong.

Februari 13, 2023, Mary Lilian Waithera, mfanyakazi wa NHIF aliyefichua sakata ya mabilioni, alianguka na kufariki ghafla katika barabara ya Kaunda, jijini Nairobi.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha alikuwa amepigwa risasi. Hata hivyo, hakuna aliyeona wala kusikia mlio wa risasi.

Ingawa hakuna pikipiki ilihusishwa moja kwa moja, wachunguzi walisema kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa mfyatua risasi kutumia pikipiki kutoroka.

Mbali na mauaji ya watu mashuhuri, visa vya uporaji mitaani vimeongezeka kwa kasi. Katika mitaa ya Nairobi kama vile Eastleigh, South B, na Donholm, wakazi wamelalamikia majambazi wanaowapora wakiwa wamepanda pikipiki.

Majambazi hawa hutumia mbinu ya kushangaza – mmoja akipora, mwenzake akiendesha pikipiki tayari kwa kutoroka kwa kasi.

Mara nyingi, wahalifu hao huvaa kofia za wanaboda boda ili kuficha sura zao, jambo linalowapa fursa ya kutoweka bila kutambuliwa.

Ingawa wengi hutumia pikipiki kujipatia riziki halali kwa kusafirisha abiria, kuna malalamishi kuwa baadhi ya wahalifu wanatumia pikipiki zilizosajiliwa kwa majina ya watu wasiohusika au kutumia nambari bandia za usajili.

Wanasheria, wahadhiri na wanafunzi wa sheria jana waliungana kumuomboleza wakili Mbobu, aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Karen, Nairobi.

Kifo chake kimeibua ghadhabu kubwa katika jamii ya wanasheria nchini, huku kukiwa na miito ya haki kutendeka haraka.

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), Nelson Havi, alimkumbuka Mbobu kama mtu mpole, mnyenyekevu na aliyekuwa rahisi kuelewana naye.

Wakili Wahome Thuku alimkumbuka kama mhadhiri makini, mkali lakini mwenye maarifa ya kipekee, aliyefundisha masomo ya Evidence I na II katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Wanafunzi wengi walifeli vipengele hivyo kwa sababu Bw Mbobu alikuwa mtu wa viwango vya juu,” alisema Thuku.

Rais wa sasa wa LSK, Faith Odhiambo, alimtaja marehemu kama nguzo muhimu katika taaluma ya sheria nchini Kenya.

“Kupitia taaluma yake pana na utumishi wake wa dhati, Bw Mbobu alitoa mchango mkubwa katika sheria na utawala nchini,” alisema Bi Odhiambo.