Kuweni mabalozi wa SHA, katibu ahimiza vijana
KATIBU wa Wizara ya Afya, Raymond Omollo amewahimiza vijana kujisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na kuipigia debe katika jamii zao.
Kulingana naye, SHA ni kielelezo bora kuhusu jinsi sera ya kibunifu zinaweza kusuluhisha changamoto zinazokabili taifa na ulimwengu kwa jumla.
Alisema Mamlaka hiyo ni moja kati ya miradi kabambe ya serikali inayodhamiriwa kufanikisha mabadiliko zaidi na imeundwa kwa namna ya kumwezesha kila Mkenya kupata huduma bora za afya pasipo kusambaratika kifedha.
“Kwa miaka mingi, familia zimelazimika kufanya harambee au kuuza ardhi ili tu kumudu kugharamia matibabu. Hayo yatafika kikomo na SHA,” alisema Dkt Omollo Jumatatu katika warsha ya ngazi za juu ya vijana Kisumu.
“Kama una mapato unachangia kiasi kidogo. Kama hauna, serikali inaingilia kati. Ni rahisi hivyo.”
Kando na kutoa bima ya huduma za afya, Dkt Omollo alisema SHA itawezesha vilevile kuunda nafasi za kazi katika sekta ya afya ikiwemo huduma ya afya kwa jamii, matibabu kupitia simu, afya ya akili, biashara kuhusu afya bora na ubunifu unaohusu afya kidijitali.
Aliwahimiza vijana kujisajili na pia kuwa mabalozi wa vuguvugu la SHA katika jamii zao akisisitiza kwamba Mamlaka hiyo ni “zaidi ya kupata matibabu.”
“Ni mkondo unaowezesha hadhi kiuchumi na kuwapa vijana nafasi ya kujenga taaluma huku wakilinda maisha,” alisema.
Alipuuzilia mbali alichotaja kuwa “habari za kupotosha kuhusu SHA” akitahadharisha vijana dhidi ya “kulaghaiwa na dhana zinazochochewa kisiasa, propaganda na uvumi.”
“Amini vituo rasmi. Ulizeni maswali. Shirikisha. Lakini usiruhusu uongo ukunyime maendeleo,” alisema.
Alisifu ubunifu, uwezo na ustahimilifu wa vijana Wakenya lakini akasisitiza ni sharti wajikakamue ili wapige hatua.
“Tuna kizazi cha watu wachanga wenye maono. Lakini ahadi hiyo ni sharti iambatane na nidhamu, ukakamavu na ujasiri.”
“Kuwa mchanga sio sababu. Ni manufaa. Yatumie kwa busara. Shughuli zina anayeziunga mkono, ni wakati wa kusonga mbele.”
Kuhusu uongozi, Dkt Omollo alifafanua kinachohitajika zaidi ni kusuluhisha matatizo badala ya siasa na kushikilia tu afisi za umma.
“Ni kuhusu kuanzisha biashara ya afya, kilimo biashara, kuendesha Sacco ya bodaboda, au kuwapa mwongozo wenzenu. Kuna njia nyingi za kuongoza na kenya inazihitaji zote.”
Alisema barabara kuu ya kidijitali na nyumba za bei nafuu, kando na kuwa mipango ya maendeleo, ina umuhimu zaidi kwa kuunda ajira akihimiza vijana kuambatisha ujuzi wao na miradi ya kitaifa inayopatiwa kipaumbele.
“Inahusu kukabiliana ana kwa ana na ukosefu wa ajira. Sio tu kusambaza intaneti na makazi.”
Warsha hiyo ilileta pamoja makundi ya vijana, wafanyabiashara wa mashinani, viongozi wa jamii na wasimamizi kutoka Kisumu.
Katibu alitoa ufadhili wa Sh500,000, matatu, pikipiki 10, tuktuk tano huku akisisitiza kwamba serikali imejitolea kuunga mkono miradi ya vijana na wanawake mashinani kupitia ufadhili na kuwaimarisha kiuchumi.
Alisema badala ya kuangazia tu malengo ya kitaifa, mtindo wa uongozi wake Rais William Ruto unapatia kipaumbele vijana na kuboresha maisha mashinani kupitia mpango wa maendeleo kutoka mashinani (BETA).
Alitaja nyumba za bei nafuu, teknolojia ya dijitali, mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya anga, kilimo na MSME, kuwa mipango inayoendeshwa na serikali inayolenga vijana.
“Sekta hizi zimeteuliwa kwa makini kwa sababu zinaashiria nyanja muhimu ambazo hazitatumiwa kikamifu nchini. Zinaonyesha jinsi vijana wetu wanaweza kuongoza, kuunda ajira na ubunifu,” alifafanua.
“Serikali inatekeleza wajibu wake kwa kuunda miundomsingi, kuongeza ufadhili, kuzindua tasnia za kidijitali na kondoa vikwazo. Lakini sasa tunahitaji nguvu za vijana. Tunahitaji maarifa, ujuzi na ari yenu.”