Kwa kaunti hizi tano, kuuzia bidhaa au huduma ni sawa na ‘hukumu ya kifo’!
RIPOTI mpya imetaja Nairobi, Kilifi, Kiambu, Machakos na Narok kama kaunti ambazo kufanya biashara na wakandarasi na wauzaji wa bidhaa ni sawa na “hukumu ya kifo”, kutokana na kucheleweshwa kwa malipo kwa muda mrefu.
Ripoti ya hivi punde ya Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o, imebaini kuwa kaunti 47 zinadaiwa na wakandarasi na wafanyabiashara jumla ya Sh 177 bilioni.
Kaunti hizo tano zilitajwa kuchangia zaidi ya asilimia 61 ya jumla ya madeni haya ikiwa ni sawa na Sh109 bilioni kufikia Septemba 30, 2025.
Serikali za kaunti zinadaiwa Sh171 bilioni huku mabunge ya kaunti yakidaiwa Sh5.55 bilioni.
Kaunti ya Nairobi chini ya Gavana Johnson Sakaja inaongoza kwa kuwa na madeni mengi ya Sh82.8 bilioni ambapo Sh62.3 bilioni ni madeni ya tangu jadi yaliyorithiwa kutoka kwa utawala uliotangulia.
Serikali ya sasa imelimbikiza Sh20.5 bilioni katika kipindi cha miaka mitatu.
Kaunti ya Kilifi chini ya Gavana Gideon Mung’aro inafuatia kwa deni la Sh9.6 bilioni, ambapo Sh8.2 bilioni ni deni la utawala wa sasa.
Kaunti ya Kiambu inadaiwa Sh6.4 bilioni, huku deni la zaidi ya Sh2.3 bilioni likiwa la chini ya mwaka mmoja wa utawala wa Gavana Kimani Wamatangi.
Machakos, chini ya Gavana Wavinya Ndeti, ina madeni ya Sh3.1 bilioni tangu alipoingia afisini.
Kaunti ya Narok inadaiwa zaidi ya Sh5 bilioni, huku Gavana Patrick ole Ntutu akirithi deni la Sh265 milioni pekee.
Kisheria, madeni yote yanapaswa kupewa kipaumbele katika mwaka wa kifedha unaofuata, lakini kaunti nyingi hazijazingatia agizo hilo.
Uchambuzi wa madeni unaonyesha kuwa Sh46.83 bilioni (asilimia 26) ni ya chini ya mwaka mmoja, Sh24.12 bilioni (asilimia 14) ni ya kati ya mwaka mmoja na miwili, Sh19.62 bilioni (asilimia 11) ni ya kati ya miaka miwili na mitatu, huku Sh85.15 bilioni (asilimia 48) yakiwa ya zaidi ya miaka mitatu.
Hata hivyo, baadhi ya kaunti zimepiga hatua ya kulipa madeni.
Kaunti za Elgeyo Marakwet (Sh17.49 milioni), Lamu (Sh18.5milioni) na Turkana (Sh721 milioni) hulipa wakandarasi na wafanyabiashara kwa wakati.
Kaunti nyingine zilizo na madeni ya chini ya Sh500 milioni ni Pokot Magharibi (Sh308 milioni), Nyeri (Sh342.3 milioni), Makueni (Sh402.5 milioni), Samburu (Sh457 milioni) na Baringo (Sh477.1 milioni).
Kaunti ya Mombasa chini ya Gavana Abdulswamad Nassir haijalipa madeni iliyorithi ya zaidi ya Sh3 bilioni, lakini imelipa madeni ya kati ya miaka miwili na mitatu, na kubakisha Sh167 milioni pekee yaliyolimbikizwa chini ya utawala wa sasa.