KWS yaongeza ada za kuingia mbugani ikiwinda pato la Sh12 bilioni
SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) limeamua kuongeza ada ya kuingia katika mbuga za wanyama kama njia ya kuongeza mapato baada ya kupungua kwa mgao wa bajeti inaopokea kutoka kwa Wizara ya Fedha.
Maelezo kuhusu nyongeza hiyo yako katika mswada wa kanuni ambao KWS imewasilisha bungeni.
Iwapo Kanuni kuhusu Usimamizi wa Wanyamapori (Ada na Matozo) 2025 itapitishwa na wabunge, KWS inalenga kuzoa Sh12 bilioni zaidi kila mwaka kutoka kwa mbuga za kitaifa, hifadhi za kitaifa na hifadhi nyinginezo za wanyamapori kote nchini.
Wakati huu, KWS hukusanya takriban Sh7 bilioni pekee kama ada za kuingia katika mbuga hizo.
Kwa hivyo, kupitia kanuni hizi mpya shirika hili linalenga kukusanya angalau Sh19 milioni kila mwaka ili kuiwezesha kujitegemea kifedha.
Kujitegemea huko kutaiwezesha KWS kuajiri walinzi zaidi, kufadhili mpango wa doria angani, kuweka ua katika mbuga zake na kuboresha barabara ndani ya mbuga hizo.
Pesa hizo pia zitaisaidia kujenga vyumba vya kutumiwa na watalii ndani ya mbuga, kujenga malango zaidi na kusaidia jamii zinazoishi karibu na mbuga.
Mkurugenzi Mkuu wa KWS, Profesa Erustus Kanga, alisema kanuni hizo “hazihusu kubadilishwa kwa ada bali thamani ya utunzaji rasilimali zetu za kitaifa,”
“Tumejitolea kuhakikisha kuwa kanuni hizi zimeboreshwa, kupitishwa na kutekelezwa kupitia mchakato jumuishi,” Prof Kanga akasema.
Aliongeza kuwa mapata yatakayozalishwa kupitia nyongeza hiyo ya ada yatatumika kuboresha huduma kwa wageni katika mbuga na hifadhi.
Pendekezo hilo la kuongezwa kwa ada za kiingilio, la kwanza ndani ya miaka 18, linalenga kuwezesha KWS kuchuma Sh12 bilioni zaidi ili kufadhili shughuli zake na kukabiliana na changamoto mbalimbali ibuka.
KWS huzalisha mapato yake kupitia ada za kiingilio kwani fedha inazopokea kutoka serikali ni finyu.
Kwa mfano, katika mwaka huu wa kifedha wa 2025/2026 mgao wa bajeti kwa shirika hilo ulipunguzwa hadi Sh1 bilioni.
Aidha, Sh7 bilioni kila mwaka ambazo KWS hukusanya kutoka kwa ada za kiingilio hazitoshi kuiwezesha kuendesha majukumu yake.
Hata hivyo, sharti pendekezo hilo la kuongeza ada za kiingilio na kanuni mpya, zinahitaji kuidhinishwa na bunge kabla ya kuanza kutekelezwa.
KWS ni shirika la serikali lenye wajibu wa kutunza na kusimamia mbuga na hifadhi za wanyama nchini.
Huhakikisha kuwa sheria za utunzaji wa wanyamapori zimezingatiwa na huendesha shughuli kadhaa ikiwemo usalama katika mbuga hizo, huendesha utafiti kuhusu wanyamapori, huendesha uhamasisho kwa umma, kuhamisha wanyamapori na kuchukua hatua panapotokea migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
KWS inapendekeza kuongeza ada ya kuingia, kwa mfano katika mbunge za kitaifa kama Amboseli na Ziwa Nakuru hadi Sh1,500 kwa raia wa Kenya ana Dola 100 (Sh12,900) kwa raia wa kigeni.