LSK yalaani mauaji ya wakili mashuhuri jijini Kyalo Mbobu
Chama cha Mawakili nchini (LSK) kimelaani vikali mauaji ya kinyama ya Wakili Kyalo Mbobu, aliyepigwa risasi Jumanne jioni katika eneo la Galleria Brookside, kando ya Barabara ya Magadi jijini Nairobi.
Katika taarifa kali iliyotolewa na Rais wa LSK, Bi Faith Odhiambo, chama hicho kilieleza masikitiko makubwa kufuatia mauaji hayo, kikiyataja kama tendo la kikatili na la kupangwa linalodhihirisha mazingira hatari ambayo mawakili wanakumbana nayo kazini.
“Chama cha Mawakili cha Kenya kinaomboleza kwa huzuni kuu mauaji ya kikatili ya Bw Kyalo Mbobu, Wakili wa Mahakama Kuu mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 30. Hili ni pigo kubwa kwa taaluma ya sheria na taifa kwa jumla,” alisema Bi Odhiambo.
Kwa mujibu wa ripoti, Bw Mbobu aliuawa mwendo wa saa moja na nusu jioni na mshambulizi aliyekuwa kwenye pikipiki, ambaye alimpiga risasi kisha akatoroka.
Bi Odhiambo aliitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuanzisha uchunguzi wa haraka na wa kina, akionya kuwa ucheleweshaji wowote utadhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za usalama.
“Tuna matarajio ya kuona kasi na weledi katika uchunguzi huu. Kinyume chake, itakuwa ni ishara ya udhaifu wa vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wao,” aliongeza.
Marehemu Mbobu alikuwa ni wakili mashuhuri, aliyewahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa Jopo la Kusuluhisha Mizozo ya Vyama vya Kisiasa na pia mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Aliwahi kufundisha sheria ya ushahidi na machapisho yake bado yanatumika sana na wanafunzi na wataalamu wa sheria.
LSK ilitumia fursa hiyo kutoa rambirambi kwa familia, marafiki na wanasheria , ikimtaja marehemu kama kielelezo cha uadilifu na uongozi bora katika sekta ya sheria.
Rais huyo wa LSK alionya kuwa ongezeko la visa vya unyanyasaji na mashambulizi dhidi ya mawakili ni tishio kwa utawala wa sheria na haki, akisisitiza kuwa mawakili wanahitaji mazingira salama ili kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.
“Hali ya sasa ambapo mawakili wanalengwa na wahalifu ni tisho kwa uhuru wa kazi yao. Tunataka waliotekeleza mauaji haya wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria,” alisema.
Bi Odhiambo pia alihusisha mauaji ya Mbobu na hali ya jumla ya ukosefu wa usalama nchini, akisema wahalifu wanaendelea kutekeleza maovu kwa ujasiri bila kuogopa sheria.