Habari za Kitaifa

Maafa ya mwanamke ndani ya shamba la Kakuzi    

April 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

UTATA umezuka kuhusu mauti ya Bi Agnes Njeri Mwaniki wa miaka 62 aliyefariki akiwa katika shamba la kampuni ya Kakuzi inayomilikiwa kwa wingi wa hisa za Uingereza.

Kampuni hiyo hudhibiti ekari 32, 900 katika Kaunti ya Murang’A, ambapo Aprili 3, 2024 Bi Mwaniki alikumbana na majeraha ambayo yaliishia kumuua.

Kakuzi imekuwa ikilaumiwa kupitia tetesi na kesi mahakamani kwamba hutekeleza visa vya dhuluma dhidi ya wenyeji ambao huingia shambani mwake bila idhini kutafuta kuni.

Ni katika hali hiyo ambapo mauti ya Bi Mwaniki yamezua gumzo, wakazi wakitaka uchunguzi wa kina ufanywe ili kubaini kama mauti hayo yangeepukika.

Miongoni mwa dhuluma ambazo husheheni ndani ya shamba hilo kwa madai ya wahasiriwa ni kuua, kubaka na kujeruhi, tetesi ambazo zilichochea maduka kadha Ulaya kususia bidhaa zake 2020.

Hata hivyo, baadaye mikakati iliyowekwa kuheshimu haki za kibinadamu.

Uchunguzi wa polisi ulionakiliwa katika kituo cha Makuyu ulisema kwamba Bi Mwaniki alikuwa ameingia katika shamba la Kakuzi kutafuta kuni za upishi.

Ripoti rasmi ambayo ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini, Bi Jane Nyakeruma ilisema kwamba Bi Mwaniki aliangukiwa na mti na akapata majeraha alipogongwa na matawi ya mti.

“Katika shamba hilo kulikuwa na wengine ambao walikuwa wakikata miti wakitumia mashine na kwa bahati mbaya akaangukiwa na mti katika ajali hiyo ya saa tano mchana katika kijiji cha Gathungururu,” akasema.

Bi Nyakeruma kupitia ripoti hiyo, alisema kwamba Bi Mwaniki aliuguza majeraha na akakimbizwa hadi hospitali ya Makuyu ambapo alipewa huduma ya kwanza na hatimaye akapelekwa hadi hospitali ya kibinafsi ya Kenol ambapo alitangazwa kuwa alikuwa ameaga dunia.

Kampuni ya Kakuzi kupitia taarifa ya Aprili 10, 2024 ilisema mauti ya mwanamke huyo yalitokana na ajali.

“Aliangukiwa na mti ambao ulikuwa ukikatwa na mwanakandarasi ambaye alikuwa amenunua miti kutoka shamba letu. Uchunguzi wetu unaonyesha kwamba mwanamke huyo hakuwa na ruhusa ya kuingia katika shamba letu,” taarifa hiyo iliyotiwa sahihi na Bw Wilson Odiyo inasema.

Bw Odiyo ambaye ni meneja wa wafanyakazi alisema kwamba mwanakandarasi huyo anashirikiana na maafisa wa polisi katika kuchunguza mauti hayo.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu anahoji ni kwa nini hakukuwa na ilani za kuwatahadharisha wapitanjia kuhusu hatari ya kukatwa kwa miti na ilikuwaje waliokuwa wakishiriki zoezi hilo hawakuwaondoa waliokuwa katika hatari ya kuangukiwa.

“Huwezi ukasema kwamba waliokuwa wakikata miti walikuwa vipofu kiasi kwamba hawakuona waliokuwa katika hatari ya kuangukiwa. Ni lazima wanaoshiriki zoezi linaloweza kuhatarisha maisha ya umma watoe ilani na wahakikishe usalama wa wote walio karibu umedumishwa,” Bw Nyutu akasema.

Ripoti ya upasuaji wa mwili iliyotolewa mnamo Aprili 5, 2024 na Dkt Kamotho Watenga imesema kwamba mauti ya mama huyo yalitokana na jeraha kwa kifua ambalo lilisababishwa na kugongwa kwa kifaa butu.

Dkt Watenga alifanya upasuaji huo na kuandaa ripoti yake katika hifadhi ya maiti ya Montezuma Monalisa iliyoko katika mtaa wa Kabati.

[email protected]