Maafisa 175 wa NPR kupiga jeki vita dhidi ya majangili Samburu
SERIKALI imetuma maafisa 175 zaidi wa polisi wa akiba (NPRs) kusaidia kupambana na ujangili ambao unaendelea kushuhudiwa Kaunti ya Samburu.
Polisi hao wa akiba walifuzu baada ya kumaliza mafunzo ya mwezi mmoja waliyopewa na maafisa wa GSU eneo la Ltungai, Samburu Magharibi.
Wanatarajiwa kusaidiana na polisi na majeshi ambayo yamekuwa yakiendesha oparesheni maeneo yenye utovu wa usalama ya Pura, Lolmolog, Longewan, Lkeek Sapuki, Malaso na maeneo mengine kwenye kaunti hiyo.
Tangu 2023, zaidi ya polisi 500 wa NPRs wamepewa ajira baada ya utawala wa Kenya Kwanza kuamua kutuma polisi wa akiba maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na ujangili na wizi wa mifugo.
Kamishina wa Kaunti ya Samburu John Cheruiyot Aprili 8, 2025 alisema maafisa wa NPR walikuwa wamepokea mafunzo spesheli ikiwemo kupewa vifaa spesheli kusaidia kupambana na changamoto za kiusalama eneo hilo.
“Watatumwa katika maeneo ambayo yameathirika ili wasaidie katika kudumisha usalama. Jukumu lao kubwa ni kuhakikisha watu hawavamiwi na mali yao pia inalindwa,” akasema Bw Cheruiyot.
Gavana wa Samburu Lati Lelelit alikaribisha uamuzi huo akieleza imani kuwa maafisa wa NPRs watasaidia kudhibiti visa vya wizi wa mifugo ambavyo vimekuwa vingi sana eneo hilo.
“Mafunzo ambayo maafisa wa NPRs wamepokea ni suluhu kwa sababu watapiga jeki juhudi za serikali ya kitaifa kupambana na ujangili,” akasema Bw Lelelit.
Kiongozi huyo aliahidi kufanya kazi pamoja na vitengo vya usalama na wanasiasa wa eneo hilo ili kusaidia kutokomeza mateso ambayo wakazi wamepitia wakivamiwa kila mara.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amesisitiza kuwa opareshini ya vikosi vya NPRs, polisi na KDF, maarufu kama Maliza Uhalifu, vitasaidia kuimarisha usalama.
Kando na Samburu, oparesheni hiyo pia inaendelezwa kaunti za Baringo, Elgeyo-Marakwet, Turkana, Pokot Magharibi na Laikipia.