Maafisa wa magereza walia wanabaguliwa kupandishwa vyeo
Tangazo la kuajiri maafisa wa Huduma ya Magereza ya Kenya (KPS) limeibua wasiwasi miongoni mwa maafisa wanaohudumu, ambao wameelezea hofu kuhusu kile wanachotaja kama ubaguzi na ukosefu wa haki katika mchakato wa kupandishwa vyeo.
Askari wa magereza wanasema vigezo tofauti vya kuwaajiri Maafisa Wakuu wa Magereza vinawapa raia wa kawaida nafasi kubwa zaidi ikilinganishwa na maafisa wanaohudumu.
Wanadai uajiri wa maafisa hao ambao unahusisha Maafisa Wakuu na Sajini Wakuu ni njama ya kuwabagua katika kupandishwa vyeo.Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa Magereza Patrick Arandu amekanusha madai hayo ya ubaguzi.
Kulingana na baadhi ya askari waliozungumza na Taifa Leo kwa sharti wasitajwe majina kwa kuhofia kudhulumiwa, baadhi ya wakuu ndani ya huduma hiyo wanadaiwa kupanga kutoa vyeo kwa jamaa zao, marafiki au watu wenye uwezo wa kifedha na uhusiano wa kisiasa, na hivyo kuwatenga maafisa wanaostahili.
Katika taarifa rasmi ya ndani iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Magereza Aprili 11, 2025 kwa wakuu wa magereza wote, askari walialikwa kuhudhuria mahojiano ya kupandishwa cheo hadi ngazi ya Afisa Mkuu wa Magereza.
Hata hivyo, tangazo la umma lililotolewa na Wizara ya Masuala ya Ndani liliwaalika raia waliotimiza vigezo kuomba nafasi za kitaaluma, wakiwemo Maafisa Wakuu na Sajini Wakuu.
Kwa waombaji kutoka umma, hitaji la chini ni shahada ya kwanza kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa.Maafisa wanaohudumu kazini wanasema huu ni ubaguzi kwani masharti yao ya kupandishwa vyeo ni magumu zaidi kuliko umma walioalikwa kuomba kazi hizo.
Afisa mmoja alisema hii ni mara ya kwanza kukumbana na masharti ya aina hiyo, na kuongeza kuwa kupandishwa vyeo katika huduma ya magereza kunapaswa kufanyika kwa utaratibu.
Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa Magereza Patrick Arandu amekanusha madai hayo ya ubaguzi.