Habari za Kitaifa

Maafisa wanasa magunia 560 ya mbolea ‘feki’ mjini Molo

March 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

MAAFISA kutoka vikosi vya usalama wamenasa magunia 560 ya mbolea inayoshukiwa kuwa bandia na iliyotarajiwa kuuziwa wakulima katika Kaunti ya Nakuru.

Hi ni baada ya maafisa hao kupata ripoti za ujasusi mnamo Jumamosi kuhusu uwepo wa bidhaa hiyo katika ghala la Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) mjini Molo.

“Maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya usalama walifika hapo na kupata shehena ya magunia 560 ya mbolea kutoka kampuni ya Kel Chemicals ya Thika ikiwa katika bohari la NCPB Molo mnamo Machi 21, 2024. Iliwasilishwa na lori la trela lenye nambari KAZ 082B na ZE6515,” ikasema ripoti ya polisi.

Mbolea hiyo ilikuwa ni ya thamani ya Sh1.4 milioni.

Kundi hilo la maafisa lilijumuisha maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Molo, Kamanda wa Kikosi cha Kulinda Miundomsingi Muhimu (Cipu), Naibu wa Kamanda wa Kaunti na wale wa Shirika la Kukagua Afya ya Mimea (Kephis). Pia walikuwepo maafisa kutoka Shirika la Kupambana na Bidhaa Ghushi (ACA).

Mshukiwa mmoja kwa jina Joseph Mbote, alikamatwa na anazuiliwa korokoroni akisubiri kuwasilishwa kortini mnamo Jumatatu.

Duru zilisema kuwa shehena hiyo ya mbolea (magunia 560) iliwasilishwa katika ghala la NCPB, Molo licha ya uwepo wa barua kutoka kwa Katibu wa Wizara ya Kilimo Paul Rono ikizuia kuwasilishwa kwa bidhaa hiyo.

Katika barua aliyotuma mnamo Machi 20, 2024, Bw Rono alisema kuwa mbolea hiyo haijaafikia viwango vinavyohitajika.