Habari za Kitaifa

Maandamano kupinga Mswada tata yachacha

Na BENSON MATHEKA June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAELFU ya vijana wamefurika katikati mwa barabara za miji nchini kushiriki maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 huku wabunge wakiendelea kuujadili bungeni.

Milipuko inasikika katikati ya jiji la Nairobi, polisi wakifyatua vitoza machozi dhidi ya vijana wanaopinga nduru na kuiba wakielezea kutoridhishwa kwao na Mswada huo.

Vijana hao wanaonekana kutiwa mori na kukamatwa kwa wenzao na maafisa wa polisi waliowateka nyara au kuvamia nyumba zao alfajiri.

Maandamano hayo ya amani yanaendelea katika miji ya Mombasa, Eldoret, Kisumu, Homa Bay na Nyahururu, miongoni mwa mingine.

Polisi wanawafyatulia vitoa machozi licha vijana hao kudumisha utulivu wakionekana kuwazuia wasielekee majengo ya bunge.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema waandamanaji wanapaswa kudumisha amani.

Kwa sasa, wanakimbizana na polisi wanaowarushia vitoza machozi huku vijana wakipiga nduru, vuvuzela na firimbi.

Maafisa wa polisi walianza kushika doria katikati mwa jiji la Nairobi kuanzia saa kumi na moja alfajri.

Polisi walifika katika barabara za Kati ya jiji kuanzia saa kumi na moja alfajiri na kupangwa katika maeneo wanayokutania vijana kuanza maandamano ambayo yamekuwa ya amani.

Hii haikuwazuia vijana kuandamana.

Barabara za jijini hazina shughuli nyingi kama kawaida ishara kuwa wafanyabiashara wanahofia kufungua biashara zao.

Kuna magari machache katikati mwa jiji kinyume na kawaida ambapo huwa ni vigumu kupata egesho.

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kikiongozwa na Rais wake Faith Odhiambo, kimewataka waandamanaji kutohusika na ghasia, uharibifu wa mali, kuchokoza polisi na kutovamia majengo yanayolindwa.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuwa waangalifu zaidi wakati huu. Wacha tuendelee kushiriki na kuwasiliana habari yoyote ambayo unaweza kuwa nayo ili kujua waliko wenzetu,” alisema.