Mabadiliko yaashiria anayeweza kuwa Mkuu mpya wa Majeshi karibuni
NA CHARLES WASONGA
RAIS William Ruto amempandisha cheo Meja Jenerali Muriu Kahariri kuwa Luteni Jenerali na Naibu Mkuu wa Majeshi (VCDF) katika mabadiliko yanayoashiria kuanza kwa mipango ya urithi wa Mkuu wa Majeshi Jenerali Francis Ogolla.
Kupandishwa cheo kwa Jenerali Kahariri kumejiri kufuatia kustaafu kwa Naibu Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Jonah Mwangi na Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu Luteni Jenerali Peter Mbogo baada ya wawili hao kufikisha umri hitajika.
Meja Jenerali David Kimaiyo Tarus ndiye atahudumu kama Kamanda wa kikosi cha Wanajeshi wa Nchi Kavu.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji, Meja Jenerali Jim Mutai, amepandishwa cheo hadi kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Naibu Chansela wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Ulinzi.
Mabadiliko hayo yalifikiwa Alhamisi katika mkutano wa Baraza la Idara ya Ulinzi chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ulinzi Aden Duale.
Rais Ruto ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, alijulishwa kuhusu mabadiliko hayo Ijumaa kabla ya kutangazwa kwa umma.
Kutokana na makubaliano hayo, Rais pia amempandisha cheo na kumteua Brigedia Thomas Njoroge Ng’ang’a kuwa Meja Jenerali.
Aidha, Ng’ang’a ameteuliwa kuwa Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Nchini.
Meja Jenerali Ng’ang’a anatoka kikosi cha Wanamaji na kulingana na taratibu jeshini, atakayeteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi Nchini atatoka kikosi hicho Jenerali Ogolla atakapostaafu mwaka 2024.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Majeshi anaweza kuongezewa muda wa kuhudumu kwa mwaka mmoja ikiwa Baraza la Ulinzi, ambalo yeye ni mwanachama, litapendekeza.
Mabadiliko mengine yaliyofanykwa ni pamoja na kupandishwa cheo kwa Meja Jenerali Juma Shee Mwinyikai kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Wanajeshi na Meja Jenerali Mohamed Nur Hassan aliyeteuliwa kuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu.
Kulingana na Kanuni iliyoanzisha na Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Daudi Tonje, almaarufu Kanuni za Tonje, wadhifa wa Mkuu wa Majeshi (CDF) huzunguka miongoni mwa vikosi vitatu vya jeshi.
Hivi ni Jeshi la Nchi Kavu, Kikosi cha Wanahewa na Kikosi cha Wanamaji au Nevi.
CDF Ogolla anatoka kikosi cha Wanahewa na mtangulizi wake, Jenerali Robert Kibochi alitoka Kikosi cha Nchi Kavu.
Hii ina maana kuwa CDF mpya baada ya Ogolla atatoka kikosi cha Jeshi la Wanamaji.
Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba mrithi wa wadhifa huo atakuwa Luteni Jenerali Thomas Njoroge Ng’ang’a ambaye ndiye Kamanda mpya wa kikosi hicho.