Mabaki ya ndovu Craig yaanza kuhifadhiwa kwa njia ya ‘taxidermy’
MABAKI ya Craig, ndovu maarufu nchini Kenya aliyekuwa akitambulika kwa pembe zake kubwa zilizokuwa zikigusa ardhi na kuwa na uzito wa zaidi ya kilo 45, umeanza kuhifadhiwa kwa njia kipekee ya taxidermy kwa madhumuni ya elimu, kisayansi, na maonyesho ya umma.
Craig, aliyekuwa akiishi katika Mbuga ya Amboseli Kaunti ya Kajiado, kwa zaidi ya miaka 50, alifariki Januari 3, 2026 akiwa na umri wa miaka 54 kutokana na kujikunja kwa utumbo mkubwa.
Upasuaji ulifanywa na madaktari wa mifugo wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) kabla ya mwili wake kusafirishwa Nairobi.
Siku 10 baada ya kifo chake, KWS imeanza mchakato wa taxidermy ambao utahifadhi ngozi na mwili wa ndovu huyo kwa umakinifu mkubwa, ili vizazi vijavyo vione na kujifunza kutoka kwa ndovu huyu wa kipekee.
“Maisha ya Craig yalithibitisha mafanikio ya juhudi za pamoja za uhifadhi. Kupitia hifadhi ya taxidermy, tunahakikisha urithi wake unaendelea zaidi ya uhai wake, ukitoa mafunzo kwa kizazi kijacho kuhusu urithi tajiri wa wanyamapori wa Kenya,” alisema Profesa Erastus Kanga, Mkurugenzi Mkuu wa KWS.
Craig atakuwa ndovu wa pili maarufu kutoka Amboseli kuhifadhiwa kwa njia ya taxidermy, baada ya tembo mwingine aliyeitwa Tim, aliyefariki 2020 akiwa na umri wa miaka 50.
Mwili wa Tim unaoendelea kuhifadhiwa sasa upo katika Makavazi ya Kitaifa ukidhihirisha historia ya ndovu wenye pembe kubwa na watulivu.
Craig alizaliwa Januari 1972 na alikuwa mmoja wa ndovu wa mwisho wenye pembe kubwa zilizokuwa zikigusa ardhi barani Afrika.
Ndovu kama hao wenye pembe za zaidi ya kilo 45 kila moja wameadimika sana Afrika.
Alilelewa kwa utulivu, akawa wa kipekee akithibitisha mafanikio ya ulinzi na ushirikiano wa jamii chini ya KWS na washirika wake wa uhifadhi.