• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mabalozi 26 wapya sasa kuanza kazi baada ya kuteuliwa rasmi na Rais Ruto

Mabalozi 26 wapya sasa kuanza kazi baada ya kuteuliwa rasmi na Rais Ruto

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amewateua rasmi mabalozi wapya 26 baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa majuma mawili yaliyopita.

Kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Ijumaa, Rais Ruto alisema maafisa hao watawakilisha Kenya kama mabalozi,  manaibu balozi na wawakilishi wa kudumu katika vituo mbalimbali vya kigeni duniani.

Majina ya 26 hao yaliwasilishwa kwa Rais mnamo Aprili 15, 2024, baada ya kupigwa msasa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni inayoongozwa na Mbunge wa Belgut Nelson Koech  kisha kupitishwa na kikao cha Bunge lote.

Miongoni mwa mabalozi walioteuliwa ni wandani wa karibu wa Rais Ruto kama vile aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi (anayeelekea Kampala, Uganda), Seneta wa zamani wa Bomet Christopher Lang’at (Abidjan, Cote d’Ivoire), aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Pokot Magharibi Lilian Tomitom (Lusaka, Zambia), aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Baringo David Kiplagat Kerich (Washington DC, Amerika) na aliyekuwa Seneta wa Kisumu Fred Outa (Cairo, Misri).

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Catherine Kirumba Karemu (London, Uingereza), Luteni Jenerali (Mstaafu) Jonah Mwangi (Tehran, Iran), Luteni Jenerali (Mstaafu ) Peter Mbogo Njiru ( Islamabad, Pakistan) na Aden Mohamud Mohamed (Jeddah, Saudi Arabia).

Orodha hiyo pia inajumuisha aliyekuwa Naibu Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kati ya 2020-2022 Carolyne Kamende Daudi (Canada), Fredrick Otieno Outa (Misri), Anne Kisaka Nangulu (Dakar, Senegal), Timothy Kaluma Mcharo (Algiers, Algeria), Jessica Muthoni Gakinya (Morocco) na Everlyne Mwenda Karisa (Havana, Cuba).

Rais Ruto pia amewateua aliyekuwa Mbunge Maalum Halima Yussuf Mucheke (The Hague, Uholanzi), aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Mashariki (EALA) Peter Mutuku Mathuki (Moscow, Russia), Moi Lemoshira (Tokyo, Japan), Kenneth Milimo Nganga (Abu Dhabi, Muungano wa Milki za Kiarabu-UAE), Abdi Aden Korio (Muscat, Oman), Gertrude N. Angote (UNEP, Nairobi), Grace Atieno Okara (Mwakilishi wa Kudumu, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi,  UN Habitat), Fancy Too (Geneva, Uswizi), David Iboko Lokemer (Dubai, Muungano wa Milki za Kiarabu-UAE) na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Turkana Erastus Lokaale ameteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN).

Naye aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano Nchini Ezra Chiloba ameteuliwa kuwa Naibu Balozi wa Kenya jijini Los Angeles, jimbo la California, Amerika.

Bw Chiloba, ambaye awali alihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), anachukua mahala pa Thomas Kwake Omolo ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu Mei 2022.

  • Tags

You can share this post!

Safisha nywele: Wigi si za kuficha nywele chafu, upara

Kocha Jurgen Klopp kagombana na hawa wachezaji sita

T L