Mabasi matupu yaelekea ‘ushago’ kuchukua abiria
NA RICHARD MAOSI
KUNA ongezeko la idadi ya matatu na mabasi matupu kutoka jijini Nairobi kuelekea mashambani kuwachukua abiria baada ya msimu wa Krismasi na sherehe za Mwaka Mpya 2024 kuisha.
Hii ikiashiria kwamba nauli zingali za juu kwa abiria wanaotaka kuingia maeneo ya mijini ambapo wamiliki wa mabasi wanafidia gharama ya mafuta ambapo bei ya petroli ni baina ya Sh211 na Sh212 kwa lita.
Hali ni kama hiyo katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi ikizingatiwa kuwa mwaka 2024 wasafiri wengi walizuru Pwani ya Kenya kusherehekea na familia zao katika hoteli za kifahari na pia katika fuo maarufu za Bahari Hindi.
Likizo ya muhula wa tatu kwa wanafunzi wa shule za msingi, upili, taasisi na vyuo vikuu inakamilika wiki ijayo.
Dereve wa Prestige Shuttle ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Elisha, anasema hivi sasa nauli zimeshuka pakubwa kwa wanaotoka jijini Nairobi ambapo wanatozwa Sh1,500 tu baina ya Nairobi na Kisumu.
Isitoshe nauli kati ya Nairobi hadi Nakuru ni Sh600 tu kwa matatu nyingi ingawa madereva wanaonya kwamba msongamano mkubwa wa watu huenda ukapandisha nauli tena.
Elisha anasema tayari baadhi ya wasafiri mashambani wameanza kukata tiketi za magari wakilenga kuwahi jijini Nairobi kuanzia mwanzoni mwa wiki ijayo.
Hata hivyo, dereva huyo anasema hashtuki kuona matatu nyingi zikichoma mafuta kutoka Nairobi zikielekea mashambani bila wasafiri.
Kwingineko katika barabara ya Nairobi-Meru hali ni tofauti kwa sababu si wasafiri wengi walioelekea mashambani mwishoni mwa mwaka wa 2023.
Bw Robin Kamathi ambaye ni dereva wa MEKINA Sacco, anasema nauli imebakia kawaida kati ya Sh1,200 na Sh1,500.
Hata hivyo anasema ingawa kuna baadhi ya magari ambayo yalipandisha nauli kuanzia Desemba na hayajashusha.
Akiamini kwamba baadhi ya magari ya PSV hayapo tayari kushusha nauli ikizingatiwa huu ni msimu wa kuvuna.