Habari za Kitaifa

Macho yote kwa Tanzania leo huku wanaharakati wa Kenya nao wakipanga kuzidisha shinikizo

December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUKU macho yote yakiwa kwenye maandamano yanayotarajiwa Tanzania leo, wanaharakati wa Kenya nao wanapanga kuandamana katika ubalozi wa taifa hilo nchini.

Wanaharakati hao jana walimfahamisha Kamanda wa Polisi wa Nairobi George Sedah kuwa wanapanga kuandaa maandamano kwenye ubalozi wa Tanzania.

Barua kwa Bw Seda ilikuwa imetiwa saini na Nicholas Oyoo ambaye ni Katibu wa Vuguvugu la Free Kenya Movement.

Rais wa vuguvugu hilo, Bob Njagi, Mwanaharakati wa Vocal Afrika, Ojiro Odhiambo na aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana waliandaa kikao ambapo walilaani kile walichosema ni udikteta wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Prof Kibwana alishutumu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kunyamazia dhuluma zinazoendelezwa Tanzania.

“Serikali imekuwa ikiendeleza dhuluma dhidi ya raia na kuwanyaka, jambo ambalo halikubaliki kamwe. Tanzania wanahitaji demokrasia, hadhi na maisha mazuri,” akasema Prof Kibwana.

Wanaharakati hao walisimulia jinsi watu 2,000 walivyofunguliwa kesi mahakamani kuhusu ugaidi na uhaini, familia zinazosaka wapendwa wao kutishiwa maisha na mawakili wanaowatetea wanaouzuiliwa kunyakwa.

Walidai kuwa umeme kupotea na mitandao kama Meta na X kuzimwa ni kati ya mbinu zinazotumika na Tanzania kuficha ushahidi.

“Ukificha miili, kuvamia hospitali, kuwatishia viongozi wa kidini na kuhangaisha jamii, basi unaongoza kupitia uoga,” akasema Bw Njagi.

Naye Ojiro Odhiambo, ambaye alisoma taarifa ya wanaharakati hao alisema kuwa yanayoendelea Tanzania hayafai kufumbiwa macho zaidi.

“Serikali ikome kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia, kuwanyaka na pia iwaachilie wote wanaozuiliwa kisha itupe kesi ambazo zina msukumo wa kisiasa,” akasema Bw Odhiambo.

Wanaharakati hao wametoa wito kwa Rais Suluhu ajiuzulu, vyombo vyote vya usalama vivunjwe na kuadhibiwa kwa wanajeshi na maafisa wa usalama wanaohusishwa na mauaji ya raia.

“Uchungu wa raia wa Tanzania si wao pekee kwa sababu taifa moja likishabikia dhuluma na mauaji basi mataifa mengi nayo yatafuatilia,” akasema Bw Oyoo.

Maandamano yanayotarajiwa leo Tanzania yameingiza serikali baridi na kuchangia maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo kufutiliwa mbali.

“Jambo kama hili halijawahi kutokea mahala popote Afrika. Iwapo mwanzilishi wa Tanzania Julius Nyerere atafufuka leo, atarudi alikotoka kwa sababu hatua hiyo itamsikitisha mno,” akasema Prof Kibwana kuhusu kufutiliwa mbali kwa sherehe.