Habari za Kitaifa

Mackenzie alitukana wafuasi waliochelea kuua watoto kwa mfungo, shahidi asema

Na BRIAN OCHARO September 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MHUBIRI tata Paul Mackenzie aliwatukana wafuasi wake waliokuwa wakinung’unika walipoambiwa wawanyime watoto wao chakula ili wafe huku akidai kuwa angepepereka hadi mbinguni, mahakama imefahamishwa.

Shahidi mmoja ambaye alikuwa katika msitu wa Shakahola wakati wa mkasa huo alisema wazazi wengi waliona vigumu kuangamiza watoto wao kwa kuwanyima chakula.

“Mackenzie alifanya mkutano ambapo alitangaza kuwa mfungo uanze na watoto. Baada ya mkutano huo, wafuasi wengine walianza kunung’unika wakisema ni ngumu kwa mzazi kuua mtoto wake akiona, lakini Mackenzie aliwaita wapumbavu,” shahidu huyo aliambia Hakimu Mkuu Alex Ithuku.

Aliendelea kusema kuwa Mackenzie alielezea wazazi waliokuwa wakinung’unika kuwa kuua ni kudunga mtu kwa kisu ama kumnyonga hadi afe, lakini kumnyima mtoto chakula mpaka afariki ni upendo kwa sababu ataenda mbinguni.

Alisema kuwa Mackenzie alishauri wafuasi wake kwa kunukuu haya katika Bibilia ampapo Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake kuwa mtu anayempenda ataichukia nafsi yake kwa ajili yake (Yesu).

“Kutokana na ushauri huu, akina mama wengi walianza kunyima watoto wao chakula na mwezi huo wa Januari 2023, takriban watoto wanane walifariki katika msitu wa Shakahola,” alisema shahidi huyo akiongozwa na kiongozi wa mashtaka Jami Yamina na wenzake Betty Rubia na Yassir Mohamed.

Japo hakukumbuka majina ya watoto waliokufa, shahidi huyo alisema alihudhuria mazishi ya karibu kila mtoto aliyefariki wakati huo.

Alisema Mackenzie alihudhuria na kuongoza mazishi hayo mwenyewe katika mwezi wa Januari 2023.

“Aliwasifu waliokufa akiwaita mashujaa waliosulubishwa na kusema walikuwa wakiketi na Yesu wakati wa mazishi . Niliona makaburi ya wafu yakichimbwa huko katika msitu wa Shakahola,” alisema

Vile vile, shahidi huyo alieleza mahakama kuwa Mackenzie aliwaambia mwezi wa Januari 2023 katika maombi ya Jumamosi kwamba Yesu alikuwa anawasubiri, na kuwa hata kama wangejitakasa bado wangezidi kufanya dhambi wakiwa humu duniani.

“Kisha alitueleza tuingie kwa maombi na tufunge hadi tufariki twende tukamuone Yesu. Maombi ilikua ni jina nyingine ya kufunga ama kujinyima chakula hadi kufariki, na wazazi walipewa jukumu la kuweka wanao kwenye maombi, ikiwa na maana ya kuwanyima chakula na maji mpaka wafariki,” alisema

Pia, alielezea kuwa Mackenzie aliwatangazia kwa mkutano kwamba ili wafe haraka na kumuona Yesu, wasile, wasinywe hata maji, wasioge, wasipige meno mswaki na wakae kwenye joto jingi.

“Alituelezea kuwa tutakula na kuoga mbinguni baada ya kufariki na kufafanua kwamba watakaoanza kufunga ni watoto, kisha vijana, akina mama halafu wanaume,” alisema.

Alisema kuwa mwili wa aliyefariki ungeingizwa kwenye kaburi lililochimbwa karibu na nyumba walimoishi, na kuzikwa ukiwa umefungwa kwa gunia ama shuka kama vile Yesu na Lazaro walivyozikwa bila jeneza kulingana na Biblia.

Wachimba kaburi walikuwa wanatumia sepetu, jembe na shoka.

Baada ya mazishi, shahidi alisema kaburi lilikuwa linatandazwa mchanga na mara mingi kupandwa mboga juu ili isijulikane kwa urahisi kwamba mwili wa binadamu ulikuwa umezikwa katika sehemu hiyo.

“Nilichoka kufunga lakini mamangu alinisihi nivumilie kwa sababu nilikuwa tayari nimefika kwenye mlango wa mbinguni,” alisema alipohojiwa na wakili wa Mackenzie Bw Lawrence Obonyo.

Alielezea mahakama kwamba Mackenzie aliwatishia kuwa kama msichana wake mwenye umri sawa na wao angekufa mbele yao basi mbinguni wasahau kuingia .

“Pia alielezea kwamba kama mkewe angefariki mbele ya akina mama wengine, basi hao hawatauona ufalme wa mbinguni. Isitoshe, aliambia wanaume wangine hawangeona ufalme wa mbinguni ikiwa yeye kama kiongozi wao angetangulia kufa ,” alisema

Shahidi huyo aliendelea kusema kuwa Mackenzie aliwaambia kuwa baada ya watoto wengine wote kufariki, ingekuwa zamu ya watoto wa Mzee Smart Mwakalama, wakifuatwa na watoto wake.

Mackenzie na wenzake 94 wameshtakiwa kwa makosa 283 ya kuua bila kukusudia.

Wanadaiwa kuwaua zaidi ya wafuasi 429 wa kanisa la Good News International katika msitu wa Shakahola.