• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Mackenzie aomba apunguziwe mashtaka kutoka 191 hadi 12

Mackenzie aomba apunguziwe mashtaka kutoka 191 hadi 12

NA ALEX KALAMA

MHUBIRI wa Kanisa la Good News International Paul Mackenzie na wenzake walioshtakiwa pamoja naye kwa makosa 191 ya mauaji ya watoto msituni Shakahola, wameiomba mahakama kupunguza mashtaka hadi 12 pekee.

Mawakili wa washtakiwa wakiongozwa na James Mouko na Wycliffe Makasembo, mawakili hao waliambia Mahakama Kuu ya Malindi kwamba si haki wateja wao kufunguliwa mashtaka 191.

“Sidhani itakuwa ni sawa kwa wateja wetu kushtakiwa na makosa 191. Tunaomba mashtaka haya yapunguzwe kutoka 191 hadi 12,” akasema Bw Mouko.

Mawakili wa upande wa washtakiwa walisema kuwa mashtaka yote yanafanana kwani ni ya mauaji japo hayaelezi majina, umri wa waathiriwa na mahali ambapo mauaji hayo yalitekelezwa.

Mhubiri Paul Mackenzie akijadiliana na wakili wake. PICHA | ALEX KALAMA

Waliitaka mahakama kutupilia mbali mashtaka hayo.

Aidha viongozi wa upande wa mashtaka wakiongozwa na Victor Mule, wameitaka mahakama kutupilia mbali ombi la washtakiwa, wakisema kuna ushahidi wa mashtaka zaidi ya 12 na hivyo kesi iendelee kusikilizwa na kuamuliwa.

Jaji Mugure Thande alisema kuwa atatoa uamuzi wake wa ombi la upande wa washtakiwa mnamo Mei 17, 2024.

Awali kabla jaji kuingia kortini Alhamisi, Bw Mackenzie alizua kioja na kuwakemea maafisa wa magereza, akidai wanamnyima uhuru wa kuzungumza na washukiwa wenzake.

“Sio sawa hiki kitu ambacho mnakifanya… mbona mnanizuia kuongea na washtakiwa wenzangu? Huu ni ukiukaji wa sheria. Nizuilieni kwa gereza na hata kwa gari mkitaka lakini hapa mahakamani hatua hiyo sio sawa,” akasema Bw Mackenzie.

Tukio hilo lilijiri baada ya baadhi ya maafisa wa magereza waliokuwa mahakamani kuketi katikati ya Bw Mackenzie na washukiwa wenzake hivyo kumzuia mhubiri huyo kuzungumza na washukiwa wenzake walioshtakiwa pamoja naye.

Hatua hiyo yao ilimkera Bw Mackenzie.

  • Tags

You can share this post!

Safu yote ya Seneti kusikiliza kesi dhidi ya Dkt Monda

Magaidi wawili kukaa jela miaka 19 kwa kupatikana na silaha...

T L