Mackenzie kufunguliwa mashtaka ya mauaji
NA WANDERI KAMAU
NI rasmi sasa mhubiri Paul Mackenzie ni miongoni mwa watu 95 watakaofunguliwa mashtaka ya mauaji, kutokana na vifo tata vya zaidi ya watu 400 katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.
Kwenye taarifa Jumanne, Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (ODPP) ilisema kuwa baada ya uchunguzi wa kina, imebaini kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka watu hao.
“Baada ya kumaliza uchunguzi wake, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilitukabidhi faili za uchunguzi huo, kubaini ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka washukiwa. Baada ya kutathmini kwa kina ushahidi uliowasilishwa kwetu, tumeridhika kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki watu hao 95,” ikasema afisi hiyo.
Kulingana na mkurugenzi huyo, washukiwa hao watafunguliwa mashtaka ya mauaji, mauaji bila kukusudia na kuwashambulia watu na kuwajeruhi kwenye miili yao.
Washukiwa pia watafunguliwa mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya jinai, uenezaji wa itikadi kali, kutoa usaidizi kwenye uendeshaji wa kitendo cha ugaidi na kuwa na maandishi yanayohusiana na kitendo hicho cha kigaidi.
Zaidi ya hayo, washukiwa watakabiliwa na mashtaka ya kuwadhulumu watoto kinyume na Sehemu 25 (3) ya Sheria ya Watoto na kuwanyima watoto haki ya elimu.
Kwa wakati ambao kesi yake imekuwa ikiendelea mahakamani, mhubiri huyo amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia yoyote.
DPP alitoa agizo washukiwa hao wafikishwe mahakamani mara moja ili kufunguliwa mashtaka.