Habari za Kitaifa

Mackenzie, wenzake 29 wakana kuhusika na vifo vya watoto 191

February 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA ALEX KALAMA

MHUBIRI tata Paul Mackenzie na wenzake 29 wakiwa mbele ya Mahakama Kuu ya Malindi wamekanusha mashtaka ya mauaji ya watoto 191 yaliyotokea msituni Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Bw Mackenzie na wenzake 29 ambao walishtakiwa Jumanne mbele ya jaji wa mahakama kuu ya Malindi Mugure Thande.

Idadi hiyo ya washtakiwa ilipungua baada ya mshtakiwa mmoja kwa jina Evans Kolombe Sirya, kuondolewa kwa muda katika kesi hiyo ambapo hakushtakiwa kwa sababu mahakama hiyo ilielezwa kuwa ni mgonjwa.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Victor Mule uliambia mahakama kwamba mshukiwa Bw Sirya ana matatizo ya akili hivyo basi hawezi kushtakiwa kwa sasa.

“Tunaomba kupewa muda wa mwezi mmoja ili atibiwe,” akasema Bw Mule.

Lakini wakili wa washtakiwa Bw James Mouko alielezea mahakama hiyo ya kwamba haelewi ni kwa nini upande wa mashtaka unasema mteja wake ana matatizo ya akili ilhali anavyojua ni kuwa Bw Sirya anaugua ugonjwa wa kupooza yaani stroke.

Upande wa mashtaka uliomba kupewa muda wa siku 14 ili kuwasilisha stakabadhi zao huku mawakili wa upande wa washtakiwa wakiomba kupewa siku saba pekee kuwasilisha stakabadhi hizo.

Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa rasmi Machi 7, 2024.

Aidha, jaji wa mahakama hiyo alitoa agizo kwa usimamizi wa magereza wanakozuiliwa washtakiwa wa kike walioshtakiwa pamoja na Bw Mackenzie kuwasaidia ili waweze kunyolewa nywele zao.