Madaktari sasa watahadharisha wanaopanga kukumbatia mti wakikimbiza rekodi
JARIBIO la Jimmy Irungu kuvunja rekodi ya dunia ya saa 72 kukumbatia mti kwa muda mrefu iliyowekwa na mwanaharakati wa mazingira, Bi Truphena Muthoni, nusura limalizike kwa machozi, baada ya kuanguka katika saa ya 79, saa moja tu kabla ya kufikia lengo lake la saa 80.
Wahudumu wa afya sasa wanashauri wahusika wanaotafuta kushiriki zoezi kama hilo kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu kubaini wapo wako katika hali shwari ya kiafya kuhimili ugumu uliopo katika kibarua hicho.
Bw Irungu, 30, alijiingiza kwenye changamoto hiyo kubwa ili kuhamasisha kuhusu saratani na pia kuunga mkono uhifadhi wa mazingira.
Alianza jaribio hilo katikati ya mji wa Murang’a mnamo Januari 5, 2025, na alitarajiwa kulimaliza Alhamisi, Januari 8, 2025 asubuhi.
Hata hivyo, karibu saa kumi na nusu alfajiri, Bw Irungu alianguka na kukimbizwa hospitalini.
Hali hiyo ilisababisha hofu kubwa miongoni mwa walioshuhudia tukio hilo, jambo lililosababisha Afisa Mkuu wa Afya Kaunti ya Murang’a, Eliud Maina, kutoa taarifa akihakikisha umma kuwa Bw Irungu alikuwa akipatiwa huduma ya matibabu.
“Bw Irungu yupo hapa pamoja nasi katika Hospitali ya Rufaa ya Murang’a na anapatiwa matibabu. Wote tuombe mema kwa shujaa wetu,” Bw Maina alisema.
Katika taarifa ya baadaye, Bw Maina aliongeza kuwa Bw Irungu alikuwa akipatiwa matibabu kwa dalili za kizunguzungu, uchovu, hasira, na udhaifu wa jumla, lakini alikuwa katika hali ya utulivu na hakuwa hatarini.
“Bw Irungu ameamka, amerudiwa na fahamu na sasa yuko pamoja na washirika na mashabiki. Murang’a imeibuka mshindi,” Bw Maina alitangaza saa nne asubuhi Alhamisi.
Sasa inabaki kuonekana kama jaribio la Bw Irungu litakidhi vigezo vinavyohitajika kuvunja rekodi ya Bi Muthoni ya Guinness World Record kwa muda mrefu zaidi wa kukumbatia mti.