Madaktari watishia kugoma Krismasi
HUENDA Wakenya wakakosa kupata huduma za kimatibabu kuanzia Desemba 22, 2024 madaktari wakipanga kuanza mgomo wao wa pili wa kitaifa mwaka huu katika kaunti zote 47 iwapo serikali haitashughulikia malalamishi yao.
Hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo wauguzi watagoma kuanzia Januari mwakani walivyotangaza.
Huduma za afya zitasimama katika kaunti zote hatua ambayo itawaweka wagonjwa hatarini.
Maafisa wa Chama cha Kitaifa cha Madaktari Kenya (KMPDU) waliotangaza mgomo huo, watatembelea kaunti zote 47 kuhamasisha wanachama wao kuhusu mgomo huo miezi mitano tu baada ya mgomo wa siku 56 uliokamilika Mei 8, 2024.
Katibu Mkuu wa KMDPU Dkt Davji Atellah aliomba Wakenya kujiandaa huku akilaumu kushindwa kwa Rais William Ruto kuheshimu makubaliano aliyofanya na maafisa wa chama hicho miezi sita iliyopita.
Muafaka wa kurejea kazini ulipaswa kutekelezwa Septemba 1, 2024, kufuatia mazungumzo ya muda mrefu kati ya KMDPU, serikali ya kitaifa na kaunti.
Masuala muhimu ambayo madaktari hao wanafuatilia ni pamoja na kuongezwa mishahara, utoaji wa bima ya matibabu kwa madaktari, kupandishwa vyeo, utekelezaji wa matakwa yaliyoainishwa katika Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja wa mwaka 2017 (CBA) na ukiukaji wa malipo ya madaktari bingwa ambao ulipunguzwa kwa asilimia 70.
Mengine ni pamoja na malipo ya malimbikizo yanayodaiwa na madaktari wakuu na madaktari wengine wote pamoja na wasajili ambao wana kazi nyingi katika hospitali za Level 6.
Akizungumza alipokutana na madaktari wanaofanya kazi katika Kaunti ya Kakamega, Dkt Atellah alisema wanarejelea hatua kali zaidi kuliko hapo awali baada ya kufanya mazungumzo na serikali na kutia saini fomula ya kurejea kazini ambayo bado haijaheshimiwa.
“Tulijadiliana na serikali na kufikia mwafaka lakini hakuna kilichotekelezwa kwa yote tuliyokubaliana. Wizara ya Afya inajua ni kiasi gani daktari anatakiwa kupata, ni kiasi gani kila daktari wa ndani anatakiwa kulipwa na ni juu yao kutekeleza hili. Muda umepita na hakuna kilichotekelezwa – ndiyo maana tutarejea barabarani,” alisema Dk Atellah.
“Kama vile serikali ya kitaifa, hakuna serikali moja ya kaunti ambayo imeonyesha kupendezwa na matakwa yetu. Tunaomba tu serikali ya juu na ya kaunti kuweka pesa kwenye akaunti za madaktari na kutekeleza makubaliano,” akaongeza Dkt Atellah.
Wameshikilia kuwa watabadilisha tu azimio lao ikiwa ngazi zote mbili za serikali zitatekeleza matakwa yao.
Mwenyekiti wa KMPDU eneo la Magharibi Joseph Makomere alishutumu serikali kwa kukosa kutenga pesa kwa shughuli zingine ambazo sio muhimu ili nchi isonge mbele.
Imetafsiriwa na Winnie Onyando