Habari za Kitaifa

Maelfu ya wamiliki wa ploti miji ya Kajiado kupata hati miliki

Na STANLEY NGOTHO December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Maelfu ya wakazi wa mijini katika Kaunti ya Kajiado watanufaika na hati mpya za umiliki wa ploti kufuatia mageuzi mapya ya ardhi yanayolenga kukomesha visa vya ulaghai wa ardhi ambavyo vimekuwa vikichochea migogoro kwa miaka mingi.

Mpango huo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Kajiado na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) utawezesha jumla ya ploti 36,800 katika miji mbalimbali ya kaunti hiyo kupatiwa hati mpya za umiliki baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

Idara ya Ardhi ya kaunti ilianza mchakato huo mwaka 2022 kwa lengo la kuharakisha utoaji wa hati hizo katika jumla ya miji 37,ikiwa na takriban wamiliki wa ploti 22,000.

Kampuni tatu binafsi zilipewa jukumu la kutekeleza mchakato huo wa utoaji hati — kila moja ikipewa miji mahususi. Kati ya ploti 8,000 za awamu ya kwanza, mji wa Kajiado (Awamu ya Pili) una ploti 2,597, Kitengela Noonkopir ploti 2,529, Namanga 1,676, Bulbul 376, Loitokitok 259 na Kimuka 169.

Awamu ya kwanza ilizinduliwa Jumanne, ambapo Gavana Joseph ole Lenku na Afisa Mkuu Mtendaji wa NLC, Bi Kabale Tache, walianza kutoa hati kwa wamiliki wa ploti katika Noonkopir, Bulbul, Namanga, Isinya, Loitokitok na Kajiado.

Walionufaika ni wale waliokuwa na barua halali ambazo zilithibitishwa miaka kadhaa iliyopita kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Gavana Lenku alisema utoaji wa hati hizo ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya ardhi inayokua kwa kasi katika kaunti hiyo.

“Tulipoingia ofisini tulikuta ploti zilikuwa na umiliki mara mbili au zaidi, na kuhatarisha maisha ya watu kwa kupeleka migogoro hiyo mahakamani. Hatua yetu ya kwanza ilikuwa ni kufanya uthibitishaji madhubuti kubaini wamiliki halali,” alisema.

Aliongeza kuwa hatimiliki hizo zitaongeza thamani ya uwekezaji kwani wamiliki sasa wataweza kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa kutumia hati hizo kama dhamana.

Bi Tache aliisifu Kajiado kwa kuongoza katika mageuzi ya ardhi, hasa kupitia mfumo wa Upatanishi Mbadala (AJS) unaotumika kutatua migogoro ya ardhi ambayo ingewachukua miaka mingi mahakamani.

Kwa upande wake, Waziri  wa Ardhi , Mipangilio ya Miji, Makazi na Manispaa wa Kaunti, Bw Hamilton Parseina, alisema mchakato huo mkubwa wa utoaji hati unarejesha hadhi ya wamiliki wa ploti na kuwawezesha kiuchumi.

Wakazi wa miji walisema wamepata afueni baada ya miaka mingi ya migogoro ya umiliki.

“Hati hii imenitambulisha rasmi kama mkazi halali wa Kajiado. Sasa ninaweza kupata mkopo wa kuendeleza ploti yangu,” alisema Zakia Wangui wa Embul Bul.