Maendeleo ya wanawake Kilifi waikalia ngumu ofisi kuu
NA MAUREEN ONGALA
WANACHAMA wa Vuguvugu la Maendeleo ya Wanawake (MYWO) katika Kaunti ya Kilifi wamepinga vikali hatua ya ofisi kuu jijini Nairobi kuahirisha uchanguzi wa viongozi kwa miaka mitano mingine.
Wanachama hao walisema hatua hiyo ni kinyume na katiba ya MYWO ambayo inasema kuwa uchaguzi wa viongozi utafanyika kila baada ya miaka mitano.
Shirika la Maendeleo ya Wanawake nchini lilifanya uchaguzi wake mwaka 2014.
Hata hivyo wamemtaka Mwenyekiti wa MYWO Kilifi Witness Tsuma kujiuzulu kwa kukosa kuwatetea wanawake mashinani na kuonekana kuegemea na kufanya kazi na ofisi kuu peke yake.
Kulingana na wanachama hao, kaunti ya Kilifi imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo vita na kutoelewana baina ya viongozi, usimamizi wa mali na pesa kwa njia isiyofaa, hali ambayo imeendelea kukandamiza maendeleo ya wanawake.
Walisema kuwa suluhu ilikuwa ni uongozi mpya kupitia uchaguzi wa mwaka huu 2024.
Wito huo wa wanawake wa Kilifi ulipigwa jeki mwaka 2023 na Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa wakati alikuwa mgeni wa heshima wa hafla ya Kishutu katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi
Bi Jumwa alisema kuwa ni lazima kuwe na mabadiliko katika shirika hilo kwa manufaa ya wanawake mashinani.
Wakiongozwa na naibu wa mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Kilifi Fides Kilifi, wanawake hao waliapa kuendela na uchaguzi mkuu kama ilivyoratibiwa kikatiba.
Akizungumza na wanahabari katika bustani la Mazingira mjini Kilifi Bi Kilifi alisema uamuzi huo wa afisi kuu ni kinyume na matajirio ya wanawake wa Kilifi.
“Wanawake wa Kilifi ndiyo wataathirika pakubwa na uamuzi wa kuhairisha uchaguzi mkuu kwa sababu tuna changamoto mingi ambazo zinahitajikusuluhishwa,” akasema.
Alisema wanawake wengi walikuwa na hamu ya kujuzwa mengi baada ya mkutano wa Kila mwaka wa Maendeleo ya Wanawake uliofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya.
“Tulipotoka kwa AGM yetu jijini Nairobi, tulipata makaribisho mabaya kutoka kwa wanachama kwa sababu walitarajia tuwaeleze kuhusu mipangilio ya uchaguzi mkuu kwani tumekuwa katika uongozi kwa miaka 10 sasa bila mabadiliko,” akasema.
Alisema tangazo la mwenyekiti wa kitaifa Bi Rahab Muiu uliwavunja moyo wanawake mashinani.
Alikosoa madai ya mwenyekiti huyo kuwa waliamua kuahirisha uchaguzi kufatia changamoto zilizosababishwa na janga la Covid-19.
“Tumepitia mambo mengi tokea ugonjwa wa Covid-19 kudhibitiwa. Hata tulipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 na ikapita na hata sasa tuna ugonjwa wa macho mekundu lakini kila mtu anaendelea na shughuli zake za kila siku kama kawaida,” akasema.
Alisema kuwa wanawake katika Kaunti ya Kilifi wameamua kufanya uchanguzi mkuu.
“Maendeleo ya Wanawake Kilifi tunatangaza kuwa kama viongozi wetu wa kitaifa hawataki uchaguzi, sisi tuko tayari kufanya uchaguzi ili kuziba mapengo na tutakutana nao mwaka 2028 wakiwa tayari,” akasema.
Kiongozi maluum katika afisi ya kaunti ya MYWO Bi Esther Kache alimtaka mwenyekiti, Bi Tsuma kujiuzulu kutoka katika uongozi kwani “akina mama katika Kaunti ya Kilifi hawajafaidi lolote ndani ya miaka 10 akiwa kiongozi kwa sababu ya uongozi mbaya”.
“Maendeleo ya wanawake ni uongozi bora na maendeleo na sio siasa. Tumeghadhabishwa kwa sababu hatujaona maendeleo ndani ya miaka 10 isipokuwa kujihusisha na mambo ya siasa sana,” akasema.
Alimpongeza waziri Jumwa kwa kusimama na wanawake wa mashinani ambao wanazidi kugandamizwa kutokana na uongozi mbaya .
“Katika MYWO tunao papa na samaki wadogowadogo ambao wanamezwa na hao papa wakubwa. Tumeshindwa kutoa hesabu ya pesa zetu jinsi inavyohitajika kwa sababu hatujakuwa na mkutano wa kila mwaka kwa miaka 10,” akasema.
“Jinsi afisi yetu ya kitaifa inavyo jaza mapengo yao ndivyo wanawake wa Kilifi wameamua kuweka mambo yao sawa,” akaongeza.
Alisema baadhi ya mali imeleta utata na mizozo isiyoisha ni vipande viwili vya ardhi vinavyomilikiwa na MYWO, moja ikiwa mjini Kilifi ambayo imekodishiwa bwenyebwenye mmoja na ingine karibu na shule ya msingi ya Kibaoni nje ya mji wa Kilifi.
MYWO Kilifi pia ina akaunti kadhaa za benki na wasimamizi tofauti.
Pia alisema wangependa kujua ni wanawake wangapi ambao wamekuwa wakihudhuria mikutano baada ya kugunduliwa ya kwamba ni baadhi yao huku majina ya wengine yakiandikwa katika daftari la kuthibisha waliohudhuria.
Bi Dzidza Albert kutoka eneobunge la Kilifi Kusini alimtetea waziri Jumwa na kuitisha mabadiliko na pia kutaka afisi kuu ijieleze kuhusu matumizi ya fedha na jinsi wanavyoongoza shirika hilo.
“Tunaunga mkono Bi Jumwa na hatua yake ya kusukuma tuwe na uchaguzi.Viongozi wetu hawataki uchanguzi watafanya kazi na nani huku mashinani?Sisi tumeumua kwa pamoja kuwa tutafanya uchaguzi katika kaunti ya Kilifi,” akasema.
Mwenyekiti wa MYWO eneobunge la Kaloleni Bi Fatuma Mwachidudu alisema kuwa wanawake wamekasishwa na hatua hiyo ya kuhairisha uchaguzi kwani walitaka mabadiliko.
Alisema wenyekiti wa MYWO kati maeneo bunge wamekuwa wakifanya kazi peke yao bila kuungwa mkno na ofisi kuu ya kaunti.
“Kufatia habari kuwa hatutakuwa na uchaguzi mwaka 2024, wanachama wetu wamekasirika na sasa wadgania ya kwamba ni njama yetu ya kutaka kuendelea kubaki katika uongozi,” akasema.
Mwenyekiti wa MYWO eneobunge la Kilifi Kaskazini Bi Ephie Chari alidokeza kuwa alitemwa nje ya ofisi na ofisi ya kaunti baada ya kukosana kufuatia kutaka maswala ya kifedha na maendeleo kuwekwa wazi.
Licha ya kuwa alichaguliwa kihalali katika uchaguzi, viongozi katika Kaunti ya Kilifi walichagua wanawake wengine, ambao walichukua nafasi hiyo kinyume na sheria kwa miaka 10.
Alikosoa hatua ya ofisi ya kitaifa kuahirisha uchaguzi na kusema kuwa ni njama ya kuendelea kuwababaisha wanawake huku wakiendelea kuungwa mkono na viongozi wabaya.
“Tutafanya uchaguzi hata bila ofisi ya kitaifa kwa sababu haya yote ni kwa minajili ya maendeleo na sio mishahara,” akasema.