• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Magaidi watumia ajira kuwavutia vijana

Magaidi watumia ajira kuwavutia vijana

NA MANASE OTSIALO

MBINU za kusajili vijana kujiunga na vikundi vya magaidi Kaskazini mwa Kenya sasa zimebadilika kwa kasi huku waathiriwa wakishawishiwa na nafasi za kazi.

Wanaotumia mbinu hii wanapatikana katika sehemu za ibada hadi viwanja vya michezo kuwawinda vijana wasio na kazi.

Ripoti za siri za usalama zimeonyesha kuwepo kwa watu wanaosajili vijana kujiunga na ugaidi katika maeneo ya mijini wakilenga kaunti zote tatu za Garissa, Wajir na Mandera.

Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi alifichua habari hizi za ujasusi za idara za usalama katika eneo hilo mwishoni mwa juma.

Mkuu huyo wa kaunti ya Wajir alifichua kuwa kuna harakati za kuwasajili magaidi Kaskazini mwa Kenya na watu wanaojifanya kusaidia vijana kupata nafasi za kazi za kijeshi nchini Syria, Israeli, na Urusi.

Kulingana na Gavana Abdullahi, mbinu hizi za kusajili magaidi zinadaiwa kufichwa kama fursa za kazi nchini Syria, Israeli na Urusi, huku ukweli ukiwa, vijana hao wanashawishiwa kujiunga na makundi ya magaidi kama vile Al-Shabaab na ISIS.

“Tunawaomba vijana wetu wasikubali kulaghaiwa au kushawishiwa na vitu vizuri ambavyo havipo; tunawasihi wasijiunge na vikundi vya magaidi iwe ni Al Shabaab, ISIS au aina nyingine ya vikundi vya kigaidi,” alisema gavana Abdullahi.

Aliongeza, “Inasikitisha kwamba vijana kutoka eneo hili wanatapeliwa kwamba kuna nafasi za kazi za kuenda kupigana nchini Urusi na Syria.”

Gavana Abdullahi, ambaye pia anahudumu kama makamu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG), aliwaonya wanaoendesha usajili huo na watu wanaoendesha itikadi kali kwamba serikali ya Kenya inafahamu shughuli zao na itachukua hatua madhubuti dhidi yao.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge afadhili wasichana waliojifungua kurejelea masomo

Junior Starlets wajifua kwa mechi dhidi ya DRC

T L